Saturday, 19 November 2016

KLABU YA ROTARY YA OYSTER BAY YASHIRIKIANA NA WADAU KUTOA UFADHILI WA ELIMU KWA WANAFUNZI WA VYUO


Wanafunzi 20 kutoka vyuo mbalimbali hapa nchini wamepata ufadhili wa elimu unaofikia jumla ya Tshs Milioni 70 kutoka Klabu ya Rotary ya Oyster Bay, fedha zilizokusanywa kutokana na michango ya makampuni na watu binafsi.

Lengo la mradi huu ni kutoa msaada wa kifedha kwa wanafunzi wa Kitanzania wenye alama za juu kimasomo na waliopata nafasi za kujiunga na vyuo lakini wakakosa fedha za kulipia masomo.

Wanafunzi hao walikabidhiwa hundi za malipo katika tafrija fupi iliyofanyika tarehe 18 November katika mgahawa wa Waterfront uliopo Slipway jijini Dar es Salaam. Tafrija hiyo iliandaliwa kwa lengo la kuadhimisha miaka 100 ya mfuko wa Rotary ambapo fedha zilizochangishwa katika hafla hiyo zitawekwa kwenye mfuko huo wa Rotary ujulikanao kama Rotary Foundation.

Rotary Foundation iliyoanzishwa miaka 100 iliyopita ina lengo la kuwawezesha wanachama wa Rotary duniani kote kukuza amani kwa kuboresha afya, kusaidia elimu na kutokomeza umasikini. Mradi wa Klabu ya Rotary Oyster Bay wa ufadhili wa masomo unaenda sambamba na juhudi za Rotary International za kusaidia elimu.

Mradi wa ufadhili wa masomo katika Klaby ya Rotary ya Oyster Bay ulianza mwaka 2010 na wanafunzi wawili kwa msaada wa mfadhili mmoja. Katika kipindi cha miaka mitano, mradi huu umefanikiwa kuwa mradi mkubwa zaidi ukilinganisha na miradi mingine inayofanywa na klabu hiyo. Mwaka huu, klabu ya Rotary ya Oyster Bay imetoa ufadhili kwa wanafunzi 20 kwenye aina mbalimbali za masomo ikiwemo uhasibu, uhandisi, udaktari na sheria na inajivunia kuanza kuona matunda yake ambapo mmoja wa wanafunzi hao amehitimu na kuanza kazi ya udaktari.

Wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali nchini Tanzania hutuma maombi ya ufadhili na mchakato wa kina hufanyika ili kuchagua wanafunzi wanaokidhi vigezo. Maendeleo ya wanafunzi wanaochaguliwa kupata ufadhili huangalia kwa ukaribi ili kubaini kama wanastahili kuendelea kupata ufadhili wa masomo katika mwaka unaofuata.

Mradi huu wa ufadhili Kwa wanafunzi unawezeshwa na michango kutoka kwa makampuni na watu binafsi ambapo mwaka huu michango imetoka Karimjee Scholarships, Karimjee Jivanjee Scholarships, D.B Shapriya Scholarships, R Sheth Scholarships, K Shah Scholarships, Nasim Manji, JDC Scholarships, Eleanor and Paul Best, Diamond Trust Bank, S Rhemtullah, pamoja na Gajjar Autoworks and Premium Finishes Limited.



NAIBU WAZIRI MPINA ALITOZA FAINI YA SHILINGI MILIONI THELATHINI GEREZA LA KEKO NA MILIONI ISHIRINI, KIWADA CHA MADAWA CHA KEKO, KWA KOSA LA UCHAFUZI WA MAZINGIRA.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Luhaga Mpina akifanya akipita pembezoni mwa mfereji wa maji taka, ambapo uko karibu na makazi ya watu
  Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Luhaga Mpina akikakagua uchafuzi wa mazingira unaofanywa na gereza la keko lililopo temeke jijini Dar es salaam.        
 Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Luhaga Mpina akizungumza na waandishi wa habari mapema hii jana mara baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa mazingira jijini Dar es salaam.       

 Kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Naibu Waziri Ofisi ya makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Mpina (Mb.) Amelitoza faini ya shilingi milioni thelathini  Gereza la keko kwa kosa la kutiririsha maji taka yanayozalishwa gerezani hapo  hivyo kuhatarisha maisha ya Binadamu na viumbe hai wengine.
Akiwa katika ziara nyingine ya ukaguzi wa mazingira jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri Mpina Alilitaka Baraza hilo kutoa agizo kwa mkuu wa gereza hilo litakalokuwa na maelekezo ya  kujenga miundombinu ya majitaka ambayo ni rafiki kwa mazingira sambamba na kulipa faini hiyo kwa muda uliyotajwa.
“Taasisi za Serikali zinapaswa kuwa mfano kwa kutii sheria za nchi hususani sheria ya mazingira nimeshasema mara nyingi na ninarudia hapa tena taasisi za serikali haziruhusiwi kuchafua mazingira kwa namna yoyote ile kwa mujibu wa sheria. “ alisisitiza Mpina.
Aidha Mpina ameitaka Manispaa ya Temeke kusimamia kuwa makini na zoezi la usafi wa mazingira katika maeneo ya Keko na kuwachukulia hatua wananchi wote wanaotiririsha maji taka katika mifereji ya maji ya mvua.
Akitoa ufafanuzi wa adhabu hiyo mwanasheria wa Baraza la mazingira, Suguta  Heche, amesema kuwa Tasisi za serikali na mashirika ya umma yana wajibu wa kufuata sheria za nchi hususani sheria za mazingira na ukiukwaji wa sheria hizo utaambatana na adhabu kama zinatolewa kwa mashirika na makampuni binafsi.
Awali Naibu Waziri Mpina alitembelea kiwanda cha kutengeneza dawa cha Keko Pharmaceutical limited na kutoridhishwa na uharibifu wa mazingira unaofanywa na kiwanda hicho wa kutiririsha maji taka katika makazi bila kutibiwa, na kutokuwa na kibali cha utiririshaji kutoka kwa bonde na kuwatoza faini ya shilingi milioni ishirini inayopaswa kulipwa ndani ya wiki mbili, na kuelekeza usafi wa mazingira kufanyika katika mifereji ya maji ya mvua na kuwaasa wakazi wa maeneo jirani kutokutupa takataka katika maeneo hayo.
Kwa upande wake Bwana Selemani Ndugwana, Meneja uthibiti na Ubora wa kiwanda hicho cha dawa alipokea adhabu hiyo, na kusema kwamba ni kubwa sana wanaomba serikali iwapunguzie adhabu hiyo, kwa kuwa ni kosa la mara ya kwanza. Akiwakilisha wakazi wa eneo la keko mtendaji wa kata hiyo Bwana Samweli Magali alisema kero ya uchafuzi wa mazingira unaotoka kwenye kiwanda hicho cha madawa ni kubwa na ni hatarishi kwa afya za wakazi wa eneo hilo.

TAASISI YA DORIS MOLLEL YAADHIMISHA SIKU YA MTOTO NJITI KWA MATEMBEZI, VISIWANI ZANZIBAR

Washiriki wa Matembezi ya hisani ya kuadhimisha Siku ya Mtoto Njiti Duniani yaliyotaribiwa na Taasisi ya Doris Mollel wakiwa na bango lenye ujumbe wa kuadhimisha siku hiyo, iliyoadhimishwa kitaifa Mjini Unguja, Zanzibar Novemba 19, 2016. Matembezi hayo yalianzia katika Uwanja wa Amani kupitia Uwanja wa Tumbaku na kuishia Viwanja vya Maisara.
 Baadhi ya viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakijumuika pamoja Wadhamini na Waratibu wa Matembezi ya hisani ya kuadhimisha Siku ya Mtoto Njiti Duniani, wakishiriki Matembezi hayo, yalianzia katika Uwanja wa Amani kupitia Uwanja wa Tumbaku na kuishia Viwanja vya Maisara, Mjini Unguja, Zanzibar.
Brass Band ya Chuo cha Mafunzo, Zanzibar ikiongoza Matembezi ya hisani ya kuadhimisha Siku ya Mtoto Njiti Dunian,  iliyoadhimishwa kitaifa Mjini Unguja, Zanzibar Novemba 19, 2016. Matembezi hayo yalianzia katika Uwanja wa Amani kupitia Uwanja wa Tumbaku na kuishia Viwanja vya Maisara.

Mkuu wa Kitengo ya Uhusiano na Mawasiliano wa Kampuni ya Vodacom Tanzania, Jacqueline Materu akiwa pamoja na Muanzilishi wa Taasisi ya Doris Mollel, Doris Mollel pamoja na washiriki wengine katika Matembezi ya hisani ya kuadhimisha Siku ya Mtoto Njiti Duniani, yaliyoadhimishwa kitaifa Mjini Unguja, Zanzibar Novemba 19, 2016.
Mgeni Rasmi katika hafla ya Matembezi ya hisani ya kuadhimisha Siku ya Mtoto Njiti Duniani, Naibu Waziri wa Afya wa Zanzibar, Harusi Said Suleiman akitoa hotuba yake, katika hafla ya Kilele cha siku ya Mtoto Njiti Duniani, iliyoadhimishwa kitaifa Mjini Unguja, Zanzibar Novemba 19, 2016. Vodacom ndio Wadhamini wakuu walioeza kufanyikisha shughuli hiyo. Kulia ni Muanzilishi wa Taasisi ya Doris Mollel na Mratibu wa Matembezi hayo, Doris Mollel na kushoto ni Mkuu wa Kitengo ya Uhusiano na Mawasiliano wa Kampuni ya Vodacom Tanzania, Jacqueline Materu.
Mkuu wa Kitengo ya Uhusiano na Mawasiliano wa Kampuni ya Vodacom Tanzania, Jacqueline Materu akizungumza katika hafla ya Kilele cha siku ya Mtoto Njiti Duniani, iliyoadhimishwa kitaifa Mjini Unguja, Zanzibar Novemba 19, 2016. Vodacom ndio Wadhamini wakuu walioeza kufanyikisha shughuli hiyo.

Baadhi ya Vikundi vya Jogging kutoka maeneo mbalimbali Visiwani Zanzibar, wakipasha moto misuli mara baada ya kumalizika kwa Matembezi ya hisani ya kuadhimisha Siku ya Mtoto Njiti Duniani, yaliyoadhimishwa kitaifa Mjini Unguja, Zanzibar Novemba 19, 2016.






Mshehereshaji wa hafla hiyo, Mishy Bomba akiweka sawa mambo.






Mkuu wa Kitengo ya Uhusiano na Mawasiliano wa Kampuni ya Vodacom Tanzania, Jacqueline Materu akipokea


WAZIRI MWIJAGE AZINDUA RASMI KAMATI YA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA NCHINI

Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji, Mh Charles Mwijage amezindua rasmi Kamati ya Kuboresha Mazingira ya Biashara Tanzania,Kamati yenye lengo la kufanya uchambuzi wa kina wa  kufanya biashara nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kamati hiyo jijini Dar es Salaam,Waziri Mwijage amesema utashi wa Serikali ya Awamu ya Tano ni kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi  unaoongozwa na viwanda kama inavyoelekezwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.

Amesema kuwa “Uwekezaji wa mazingira bora ni zoezi endelevu hivyo kazi yetu Sekta ya Umma na Sekta binafsi ni kujipima katika maboresho”.

Katibu Mkuu-Sera,Ofisi ya Waziri Mkuu(PMO),Dkt.Hamisi Mwinyimvua amezungumzia Jitihada za Serikali kuhusu Maboresho ya Mazingira ya Biashara zilizokwisha fanyika na kuahidi kuendelea kufanyika.
 Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mh. Charles Mwijage akizungumza na Wadau mbalimbali wa Sekta ya Biashara wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Kuboresha Mazingira ya Biashara jijini Dar es Salaam.
   Katibu Mkuu-Sera,Ofisi ya Waziri Mkuu(PMO), Dkt.Hamisi Mwinyimvua akizungumzia Jitihada za Serikali kuhusu Maboresho ya Mazingira ya Biashara zilizokwisha fanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mh. Charles Mwijage akiwa katika picha ya pamoja na ziongozi mbalimbali jijini Dar es Salaam. Picha na Emmanuel Massaka, Globu ya Jamii.

WAZIRI SIMBACHAWENE AFUNGA MAFUNZO YA UONGOZI NA MAADILI YA VIJANA WAZALENDO 47 KIVUKONI JIJINI DAR ES ESALAAM


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi) George Simbachawene, akisalimiana na Katibu Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama, baada ya kuwasili Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kufunga mafunzo ya uongozi na maadili ya vijana wazalendo 47 yalifungwa chuoni hapo Dar es Salaam leo. Kulia ni Samuel Kasori, aliyekuwa Msaidizi wa Hayati Baba wa Taifa ambaye alipata fursa ya kuzungumza katika hafla hiyo kuhusu suala zima la maadili ya uongozi na uzalendo.
Kikao kifupi kikifanyika ofisini kwa mkuu wa chuo hicho 
kabla ya kwenda ukumbini.
Wanafunzi wa chuo hicho wakiwa ukumbini kwenye hafla hiyo.



Mgeni rasmi Waziri Simbachawene (wa pili kushoto) na viongozi wengine wakielekea ukumbini. Kutoka kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Filbert Sanga, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida, Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Wilson Mukama na Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Profesa Shadrack Mwakalila.
Wimbo wa Taifa ukiimbwa.
Wimbo wa Taifa ukiimbwa.
Taswira ya ukumbi wakati wa hafla hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Filbert Sanga akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndungulile akizungumza.
Mzee Samuel Kasori, aliyekuwa Msaidizi wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere akizungumza kwenye hafla hiyo.
Wahitimu hao 47 wakiwa kwenye sherehe hiyo.
Wahitimu hao 47 wakiimba wimbo maalumu.
Waziri Simbachawene akihutubia.
Muhitimu, Ebeneza Emmanuel akipokea cheti kutoka kwa 
mgeni rasmi.
Petro Magoti akikabidhiwa cheti.
Mhitimu Happiness Agathon akipokea cheti.
Mzalendo Theodora Malata akipokea cheti.
Mgeni rasmi katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali.
Picha ya pamoja na wahitimu hao.

Na Dotto Mwaibale

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi) George Simbachawene amesema ili kusimamia mabadiliko na maendeleo ya nchi na maadili inatakiwa kuwa na kiongozi mbabe na mtemi.

Simbachawene aliyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya uongozi na maadili kwa wahitimu 47 wazalendo waliyoyapata Chuo cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere Kivukoni Kigamboni jijini Dar es Salaam baada ya kumaliza kazi ya ujenzi ya kujitolea ya mwezi mmoja wilayani Mkuranga mkoani Pwani.

Alisema ili kusimamia mabadiliko na maendeleo nchi inatakiwa kuwa na mtu mbabe na mtemi na si kutegemea kundi fulani la watu kwani kwa kufanya hivyo kila kundi litahitaji kupendelewa baada ya kujiona bora kuliko jingine.

Alisema bila kuwa na viongozi wenye maadili nchi haiwezi kusonga mbele kwani tangu kuachwa kwa vijana kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambako kulikuwa kukitolewa mafunzo ya maadili athari zake zilijitokeza na ndipo kwa kipindi cha miaka 20 Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilijikuta kikivamiwa na matajiri wakitaka nafasi mbalimbali za uongozi katika ngazi za ubunge, urais na kuingia katika ujumbe wa mkutano mkuu wa chama kwa njia ya fedha.

"Napenda kusema kuwa tunahitaji mabadiliko makubwa ya kukifumua chama chetu hasa katika mfumo mzima wa kupata viongozi kwani uliopo umetufanya tupoteze baadhi ya nafasi katika majimbo na hata katika uchaguzi ndogo kutokana na mfumo mbaya tulishindwa vibaya baada ya wanachama wetu kumpigia kura mtu mwingine kwa hasira huko vikao vyote vikiendeshwa kwa misingi ya fedha" alisema Simbachawene.

Alisema ilifika kila jambo lilikuwa haliwezi kufanyika bila ya kuomba ufadhili kutoka kwa matajiri ambao wengi wao ndio hao walikuwa wakwepa kodi.

Aliongeza kuwa watumishi wa umma wamekuwa wakilalamika kuwa hali ya maisha imekuwa ngumu huku wengine wakisema hazina hakuna fedha wakati hakuna hata mwezi mmoja ambao mtumishi amekosa kupewa mshahara wake.

Alisema pengine hali hiyo inatokea kwa kuwa watumishi hao walikuwa wakitegemea kitu kingine mbali ya mshahara baada ya mianya hiyo kufungwa ndio maana wameanza kulalamika.

Simbachawene alisema awali bandarini kulikuwa na pilika pilika nyingi mlundikano wa mankotenta na magari lakini makusanyo yalikuwa hayafiki hata bilioni moja kwa mwezi lakini hivi sasa pilika pilika hizo hazipo tena makusanyo yanafikia trioni  moja hii inaonesha pamoja na kuwepo kwa pilika pilika hizo kodi ilikuwa hailipwi ipasavyo.

Alisema nchi ilifikia pabaya kwani kila sehemu kulikuwa na madalali iwe hospitali, ofisi za serikali, mahakamani na hata kupata cheo lakini hivi sasa mambo hayo yamebanwa.

 Alisema anachokifanya Rais John Magufuli ni mabadiliko ili watu waache kuishi kwa mazoea badala yake wafanye kazi ili nchi ipige hatua katika masuala yote.

Simbachawene alisema changamoto kubwa iliyopo ni kuchanganya sera za siasa na za uongozi jambo linalosabisha mambo mengine kushindindwa kusonga mbele.

Waziri Simbachawene aliwapongeza wahitimu hao kwa kuwa na uzalendo kwa nchi yao ambapo aliahidi majina yao kuyapeleka kwa Rais Dk. John Magufuli kuona jinsi ya kuwasaidia ukizingatia kuwa wote ni wasomi wa shahada ya kwanza katika ngazi ya taaluma mbalimbali na akawaomba vijana wengine kuiaga mfano wa vijana hao.

Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Profesa Shadrack Mwakalila alisema baada ya kuona mmomonyoko wa maadili miongoni mwa jamii ya watanzania hasa kwa baadhi ya viongozi chuo hicho kimeona ni vyema kurejesha tena mafunzo ya uongozi na maadili ili kupitia mafunzo hayo waweze kupunguza kama si kumaliza kabisa kasi ya mmomonyoko wa maadili iliyopo kwa sasa.