Friday, 11 August 2017

KIBITI KWA MOTO, POLISI WAUA WAHALIFU 13

WAHALIFU 13 WAUAWA KIBITI



JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI TANZANIA


 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ndugu Wanahabari
Tarehe 04.08.2017 huko eneo la Gari Bovu, kijiji cha Chamiwaleni, Kata ya Mchukwi, Tarafa ya Kibiti, Wilaya ya Kibiti, Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Jeshi la Polisi lilimkamata Abdallah Abdallah Mbindimbi @Abajani akiwa ana majeraha maeneo mbalimbali ya mwili wake akionekana kuwa alikuwa anaendelea kujitibia mwenyewe kwa njia za kificho. Mtuhumiwa huyu, alikamatwa kutokana na kuwepo kwa taarifa za kiintelijensia kuhusu yeye kuhusika na vitendo vya kufadhili, kusaidia, kuhifadhi na kushiriki uhalifu wa ujambazi maeneo mbalimbali. Mtuhumiwa alipohojiwa kuhusiana na tuhuma zinazomkabili alikubali na alionyesha dhamira ya kwenda kuonyesha Ngome yao.


Ndugu Wanahabari
Tarehe 09.08.2017 majira ya saa 21:00 Hrs (saa tatu  usiku) katika mapori ya kijiji cha Rungungu mtuhumiwa akiambatana na Askari Polisi alikwenda kuonyesha Ngome ya watuhumiwa wenzake aliokuwa anashirikiana nao kufanya uhalifu. Baada ya kukaribia eneo la tukio ulitokea upinzani mkali wa majibizano ya risasi jambo lililopelekea hata Abdallah Abdallah Mbindimbi @Abajani kujeruhiwa na risasi sehemu mbalimbali za mwili wake. Kufuatia majibizano hayo, Askari Polisi walifanikiwa kuwajeruhi wahalifu 12 (kumi na mbili. Jitihada zilifanyika kuwapeleka Hospitali majeruhi wote 13 (kumi na tatu) ingawa baadae walifariki dunia kwa nyakati tofauti wakipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutokana na kuvuja damu nyingi zilizosababishwa na majereha ya risasi sehemu mbalimbali za miili yao. Miili ya marehemu imehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Jijini Dar es salaam.
Ndugu Wanahabari
Watuhumiwa 7 (Saba) kati ya 13 (kumi na tatu) waliopoteza maisha  kutokana na majibizano ya risasi wametambuliwa kuwa ni:
1.  Hassani Ali Njame
2.  Abdallah Abdallah Mbindimbi @ Abajani
3.  Saidi Abdallah Kilindo
4.  Abdulshakuru Mohamed Ubuguyu
5.  Issa Mohamed Mseketu @Mtawa
6.  Rajabu Thomas @Roja
7.  Mohamed Ally Kadude @Upolo
Miili 6 (sita) iliyobaki haikuweza kutambulika mara moja hivyo utambuzi utaendelea huko ilikohifadhiwa Hospitalini DSM.
Ndugu Wanahabari
Vielelezo mbalimbali vilipatikana katika eneo la tukio, kama ifuatavyo:
S/N
KIELELEZO
UTAMBUZI
SILAHA, RISASI NA MABOMU
1.   
SMG = 5
Mali ya Jeshi la Polisi tukio la kupora Silaha Askari huko Mtengeni – Jaribu Mpakani
2.   
Anti Riot Gun 38mm = 2
Mali ya Jeshi la Polisi tukio la kupora Silaha Askari huko Mtengeni – Jaribu Mpakani
3.   
SAR = 1
Mali ya Jeshi la Polisi tukio la kupora Silaha Askari Polisi huko Stakishari Jijini Dar es Salaam
4.   
MAGAZINI = 2
Mali ya Jeshi la Polisi tukio la kupora Silaha Askari huko Mtengeni – Jaribu Mpakani
5.   
Risasi za SMG 158
Mali ya Jeshi la Polisi tukio la kupora Silaha Askari huko Mtengeni – Jaribu Mpakani
6.   
Bomu la kurusha kwa mkono = 1
Uchunguzi dhidi ya Bomu hilo unaendelea
7.   
Mabomu ya kutuliza ghasia = 4
Mali ya Jeshi la Polisi tukio la kupora Silaha Askari huko Mtengeni – Jaribu Mpakani
VIELELEZO VINGINE
8.   
Pikipiki  = 2
Pikipiki hizi zilitumika kuwasafirisha wahalifu hawa kwenye utekelezaji wa matukio ya uhalifu maeneo mbalimbali
9.   
Vitenge na Nguo mbalimbali
Vitenge na nguo mbalimbali viliporwa baada ya kufanya tukio la kumuua Diwani wa Zamani wa Kibwiwi
10.       
Begi = 1
Liliporwa baada ya kumuua Mtendaji wa Kijiji cha Mangwe

Ndugu Wanahabari
Kwa mujibu wa taarifa za utambuzi wa vielelezo vilivyopatikana eneo la tukio na utambuzi wa baadhi ya miili ya watuhumiwa waliofariki  inaonyesha kuwa walishiriki matukio ya uhalifu maeneo mbalimbali kama ifuatavyo:
1.          Kuua OC CID na Watumishi 2 (Wawili) wa Idara ya Maliasili katika tukio la Jaribu Mpakani – Wilaya Kibiti
2.          Kuua Askari Polisi 8 (Nane) katika tukio la Mkengeni – Wilayani Kibiti
3.          Kuua Trafiki 2 (Wawili) katika tukio la Bungu “B” – Wilaya ya Kibiti
4.          Kumuua Diwani wa Zamani CCM katika tukio la  Kibwibwi – Wilaya ya Kibiti
5.          Kuua Afisa Mtendaji,  Mwenyekiti wa Mtaa na Mkulima katika tukio la Kijiji cha Mangwi – Wilaya ya Kibiti
Ndugu Wanahabari
Wito wangu kwa Wananchi ni kuhusu mambo muhimu yafuatayo:
a.           Wananchi wote nchini kuondoa hofu ya kwamba eneo hili si salama. Nawaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi na kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu. Aidha nawaomba wananchi kutoa taarifa mara moja kwa Jeshi la Polisi  wanapohisi kuna jambo lolote wanalolitilia mashaka.
b.          Natoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Pwani, hususani maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Ikwiriri, kuendelea na shughuli zao mbalimbali za kujiletea maendeleo. Nawasihi kwa dhati kabisa waendelee kutupatia taarifa zitakazosaidia kumaliza kabisa uhalifu kwenye eneo hili. Nitumie fursa hii kuwashukuru sana wananchi wa maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Ikwiriri kwa ushirikiano mnaotupatia ambao umesaidia sana kuwadhibiti wahalifu.
c.           Mamlaka za Hospitali, Zahanati, Vituo vya Afya, Maabara za Afya ya Binadamu na Maduka ya Kuuza Dawa za kutibu Binadamu zijiepushe na utaratibu wa kutoa matibabu kienyeji au kificho kwa watu waliojeruhiwa bila kufuata taratibu za kisheria ikiwemo kupata taarifa ya Polisi “kupitia Fomu maalum ya kuruhusu matibabu (maarufu kama PF. 3)”. Wahalifu wakijeruhiwa ni lazima watafute matibabu.
Kwa hiyo idara hizi ni muhimu sana kutoa ushirikiano ili kutuwezesha kuwakamata watuhumiwa maana baadhi yao wamekutwa na majeraha sehemu mbalimbali za miili yao na walikuwa wanaendelea kujitibia kwa kificho kwa kutumia dawa za hospitali. Natoa wito kwa Mamlaka hizo kutoa taarifa mara moja kwa Jeshi la Polisi wanapoona ama kumbaini mtu ambaye ataonekana kuwa na majeraha na anatafuta tiba bila ya kufuata taratibu.    
Ndugu Wanahabari
Napenda kuujulisha Umma kwamba wapo baadhi ya Watuhumiwa, Wafadhili na Washirika wa Uhalifu na Wahalifu wa ujambazi maeneo haya ambao bado hawajakamatwa. Jambo la kufurahisha ni kwamba taarifa zao zipo kwa Jeshi la Polisi nchini na zinaendelea kufanyiwa kazi ili  waweze kukamatwa na kufikishwa kwenye mkono wa Sheria mara moja.
Natoa wito kwa wananchi ambao wanawafahamu watuhumiwa wafuatao kutoa taarifa katika kituo chochote cha Polisi ili waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria. Picha za watuhumiwa hao zitasambazwa kote nchini ili iwe rahisi kuwabaini. Majina ya watuhumiwa hao ni:
i.            Anafi Rashid Kapelo @ Abuu Mariam
ii.          Hassan Haruna Kyakalewa @ Abuu Salma @ Shujaa @ Dokta
iii.       Haji Ulatule
iv.        Shekhe Hassan Nasri Mzuzuri
v.           Rashid Mtutula

Ndugu Wanahabari
Nimalizie kwa kusema kwamba uhalifu kwenye eneo hili ni suala la muda mfupi. Na tunaendelea vizuri sana. Hali ya usalama imeimarika sana eneo hili. Nazidi kutoa wito kwa wananchi kuendelea kuliunga mkono Jeshi la Polisi ili kufikia malengo yake ya kuzuia, kubambana na kutanzua uhalifu nchini.

Imetolewa na;

Simon Nyakoro Sirro
Inspekta Jenerali wa Polisi
IKWIRIRI
10.08.2017

No comments:

Post a Comment