Tuesday, 12 July 2016

DC ASIA ABDALAH AANZA KAZI KILOLO KWA KUPIMA UKIMWI





Mganga wa kituo cha afya Kilolo Ephlon Msuva akimpima HIV mkuu wa wilaya ya Kilolo mkoani Iringa Bi Asia Abdalaha ambaye alitembelea kituo hicho kuhamasisha zoezi la upimaji VVU na kuona huduma zinazotolewa kituoni hapo .

Mkuu wa wilaya ya Kilolo Bi Asia Abdalah katikati akiwa na watendaji wa kituo cha afya Kilolo kushoto ni mganga mkuu wa kituo hicho Dr Seleman Hassan na kulia ni Ephlon Msuva.


Na MatukiodaimaBlog

MKUU mpya wa wilaya ya Kilolo mkoani Iringa Bi Asia Abdalah ameanza kazi ya kumwakilisha Rais Dr John Magufuli kwa kupima Virusi vya UKIMWI kama njia ya kuhamasisha wananchi wa wilaya ya Kilolo kupima afya zao .

Akizungumza baada ya kupima na kutembelea kukagua huduma zinazotolewa kituo cha afya cha Kilolo leo asubuhi ,mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa ni siku yake ya pili ya kuanza kazi ndani ya wilaya hiyo ya Kilolo ila mbali ya siku ya kwanza kufuatilia utekelezaji wa agizo la Rais Dr Magufuli la madawati siku yake ya pili ameamua kutembelea kituo cha afya kuona huduma zinazotolewa pia kupima HIV kama njia ya kuhamasisha jamii.

Mkuu huyo alisema kuwa mkoa wa Iringa kwa takwimu zilizopo unaonyesha kuwa ni miongoni mwa mikoa ambayo ipo juu katika maambukizi ya virusi vya UKIMWI na wilaya yake ya Kilolo ni miongoni mwa wilaya zenye maambukizi ya VVU hivyo pamoja na kutembelea na kupata maelezo ya mikakati ya wilaya katika kupambana na maambukizi mapya ya VVU amelazimika kupima VVU kama sehemu ya kuhamasisha jamii ya Kilolo na pia kuonyesha mfano kwa jamii.

“ Nawaomba wananchi wa Kilolo kujenga utamaduni wa kujua afya zao kwa kupima VVU pamoja na magonjwa mengine ambukizi ili kuwa na wananchi wenye afya bora “Alisema kuwa serikali imeweka utaratibu mzuri wa kuwapatia dawa wale wote watakaobainika kuwa na maambukizi ya VVU na kuwa lengo ni kuona hakuna mtanzania ambaye anapoteza maisha kwa kukosa dawa hizo za kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI .

Aidha aliwataka wauguzi na madaktari katika wilaya hiyo kuendelea kufanya uhamasishaji na elimu kwa jamii ili wazidi kujitokeza kuchunguza afya zao .Pia alisema amefurahishwa na mkakati wa wilaya ya Kilolo wa kujenga Hospitali yake ya wilaya katika makao makuu ya wilaya hiyo na kuwa tayari wilaya imetenga ardhi kwa ajili ya ujenzi huo .

Alisema suala la kusogeza huduma za afya karibu na wananchi ni moja kati ya sera chama cha mapinduzi (CCM) na kwa upande wake atahakikisha ujenzi huo unakamilika .

Kwa upande wake Mganga wa kituo hicho cha afya Kilolo Dr Seleman Hassan alisema wilaya hiyo imekuwa na mikakati mbali mbali ya kupambana na maambukizi ya VVU na kuwa wakati wa mbio za mwenge wilayani hapo jumla ya watu 200 walijitokeza kupima VVU na kati yao watu 19 waligundulika kuwa na maambukizi ya VVU na tayari wameingizwa katika huduma ya kupewa dawa za ARVS

No comments:

Post a Comment