Tuesday, 5 July 2016

SHIRIKA LA MADINI LA TAIFA (STAMIKO) LAANZISHA VITUO SITA VYA KUTOA ELIMU KWA WACHIMBAJI WADOGO MIKOA SITA .




Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa Stamiko Deusdedith Magala,akizugumzana na waandishi wa habari hawapo pichani juu ya wameanzisha vituo sita vya kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo katika mikoa sita,leo jijini Dr es Salaam.


Wanyakazi wa Shirika la Madini la Taifa Stamiko wakionesha jinsi walivyoimarisha usalama na uokoaji migodi,leo jijini Dar es Salaam.(Picha na Emmanuel Massaka,Globu ya Jamii)

Akizungumza katika maonyesho ya 40 ya biashara ya Kimataifa Dar es Salaam yanayofanyika katika viwanja vya sabasaba wakati wakionesha jinsi namnausalama na uokoaji unavyofanyika katika mgodi wa Biharamulo, Kaimu Mkurugenzi wa Stamiko Deusdedith Magala, alisema kuwa vituo hivyo vitakuwa katika mikoa sita kwa ajili ya kutoa mafunzo ya usalama kwa wachimbaji wadogo.

Alivitaja vituo hivyo kuwa ni Mkoa wa Kagera, Mara, Mbeya Singida Mwanza na Geita ambavyo watakuwa wanatoa elimu ya usalama kwa wachimbaji wadogo kuepuka ajali migodini.

Hata hivyo aliwataka wachimbaji wadogo kuhakikisha wanafika katika vituo vya stamiko vilivyopo karibu kupatiwa elimu jinsi ya kuepuka ajali zinazotokea migodini mara kwa mara. "Suala la usalama na uokoaji katika Migodi inatakiwa kupewa kipaumbile ili kuepuka ajali za mara kwa mara kwa wachimbaji wadogo wakielimika ajali za migodini zitaepukika,"alisema Magala.

Kwa Upande wake Mjiolojia Mkuu wa Mgodi wa Biharamulo Ayoubb Nyenzi aliyemwakilisha meneja wa mgodi wa dhahabu wa Biharamulo, Amesema Tanzania ina wataalamu wazuri wa kuchimba madini hivyo ni vyema serikali ikawapa nafasi zaidi ili kuhakikisha rasilimali hiyo inaleta manufaa zaidi hapa nchini.

Nyenzi alisema mgodi huo unashirikiana kwa karibu na jamii inayozunguka mgodi ambapo wameweza kutoa madawati 2000 kwa shule pamoja na ujenzi wa shule ya sekondari. Aliendelea kusema wameweza kufanya biashara na wananchi wanaozunguka eneo hilo kwa kuwapatia elimu ya kilimo cha mboga mboga na matunda ambapo wanauzia mgodi na wameweza kujipati milioni 2000.

Naye Mrakibu wa usalama afya na uokoaji Mgodini Fotunatus Japi, alisema suala la usalama lazima lizingatiwe hususani kwa wachimbaji wadogo na wakubwa. Alisema katika mgodi wao wa Biharamulo wamekuwa wakizingatia suala la usalama kwa kuwa iwapo majanga yakitokea kunaathiri soko la dhahabu inayotoa mgodini hapo.

Hata hivyo alisema wanatumia juhudi zote kuhakikisha hakuna majanga na pale yanapotokea kunakuwepo na uokoaji wa uhakika.

MFALME WA AFRO POP TWENTY PERCENT ARUDI KWENYE GEMU KWA KISHINDO NA SAUTI YAKE YA GHARAMA


Na Sultani Kipingo
Mfalme wa Afro Pop nchini Abbas Hamisi Kinzasa almaarufu kama 20% (Twenty per Cent) anavunja ukimya na kurejea kwa kishindo kwenye anga ya muziki,  huku akiwa msanii wa kwanza kusaini mkataba na lebo mpya ya KOMBINENGA inayoendeshwa na producer nguli John Shariza a.k.a Mann Water.
Twenty Percent, ambaye mwaka 2011 alitwaa tuzo saba za Kilimanjaro Music Awards (KTMA) kwa mpigo, huku Mann Water akisomba tuzo mara mbili mfululizo  za producer bora (mwaka 2013 na 2014), tayari amesharekodi vibao vitano na anatarajia kuachia ngoma moja mpya ya kwanza Julai 18, 2016, katika kuandaa albamu yake ya SAUTI YA GHARAMA.
"Nimerudi kuwachinja tena" anasema Twenty Per cent, akiwa anakamilisha kurekodi katika studio za Combination Sounds iliyoko Kinondoni Mkwajuni jijini Dar es salaam. "Nimerudi kurudisha sauti ya gharama  kwa jamii. Sauti inayofundisha. Sauti inayoonya. Sauti inayoburudisha. Sauti inayozengua kila mtu, " anaogeza.
Tayari Tweny Per cent ameshasaini mkataba wa miaka mitano na lebo ya KOMBINENGA, katika hafla fupi iliyofanyika Jumapili katika ofisi za Combination Sounds. Kuanzia sasa shughuli zote za msanii huyu zitasimamiwa na lebo hiyo chini ya Producer Mann Water.
Wakili msomi Iddi M. Gogo wa Alpha Attorneys ndiye aliyefanikisha zoezi hilo la kutiliana saini mkataba lililoshuhudiwa pia na meneja uzalishaji wa Combination Sounds, Rowel Moses.
"Namkubali sana Twenye Pa kwani ni msanii aliyetimia na hutumii shuruba wakati wa kurekodi maana ana kipaji cha ajabu cha kutunga akiwa wima na kukariri hapohapo", anasema Mann Water, ambaye ameshafanya kazi na  wasanii nyota kibao wakiwemo  Lady Jay Dee,  Ali Kiba, Ommy Dimpoz, Christian Bella, MB Dogg, Juma Nature, Mr Blue na wengine wengi.
 Twenty Percent alitamba sana tokea mwaka 2006 kwa wimbo wake wa "Manemane" uliomfanya ashinde tuzo ya KTM, kabla ya kuweka historia ya kusomba tuzo saba kwa mpigo mwaka 2011. wakati huo nyimbo zilizompandisha chati zilikuwa ni "Tamaa Mbaya"  na "Ya nini Malumbano" na "Maisha ya Bongo"   
Mbali na Muziki Twenye Percent pia alitamba sana kwenye tasnia ya filamu ambapo alicheza kwenye mchezo uliofahamika kwa jina lake la 20%. Baada ya hapo akaamua kupumzika kwa muda na kujishugulisha na shughuli za kilimo. "Kilimo kinaendelea vyema na sasa nimeamua kurudi kwenye gemu ili kuwachinja tena" alimalizia, akiinuka kuelekea kwake Kimzichana, Mkuranga, Mkoa wa Pwani, anakoishi.
Producer nguli wa muziki nchini John Shariza a.k.a Mann Water (chini kushoto) akiweka saini kwenye hati ya mkataba wa lebo ya KOMBINENGA kurasimisha usimamizi wa kazi za msanii Abbas Hamisi Kinzasa almaarufu kama 20% (Twenty per Cent) akishuhudiwa na Wakili msomi Iddi M. Gogo wa Alpha Attorneys  (juu kulia) aliyefanikisha zoezi hilo, pamoja na meneja uzalishaji wa Combination Sounds, Rowel Moses (juu kushoto) kwenye studio za Combination Sounds Kinondoni Studio jijini Dar es salaam.

No comments:

Post a Comment