Tuesday, 2 August 2016

MADIWANI MJI WA KIBAHA WAWAASA WATENDAJI/WATAALAMU WA HALMASHAURI KUSIMAMIA ILANI

index1Mbunge wa jimbo la  Chalinze Ridhiwani  Kikwete, akizungumza na vijana wa Chalinze Saccos iliyoanzishwa jimboni hapo ambapo Ridhiwani  ni mlezi wa saccos hiyo(Picha na Mwamvua Mwinyi)
indexMadiwani mbalimbali wa halmashauri ya Mji wa Kibaha, wakiwa katika kikao cha baraza la  madiwani ambacho kilijadili na kupitisha agenda ikiwemo taarifa ya maendeleo ya kata,kupokea taarifa ya mapato na matumizi ambapo waligomea kupitisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka jana  baada ya kubaini mapungufu makubwa.(Picha na Mwamvua Mwinyi)
……………………………………………………………………………
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
MADIWANI wa halmashauri ya Mji wa Kibaha ,wamewataka wataalamu na watendaji wa halmashauri hiyo kuwa makini katika kuandaa taarifa mbalimbali ikiwemo ya utekelezaji wa ilani ili kuondokana na usumbufu wa kufanya maboresho yasiyo ya lazima.
Wamesema taarifa ya utekelezaji wa ilani ya mwaka jana ambayo ilikuwa ikijadiliwa katika kikao cha madiwani kilichofanyika ,kujadili mambo ya maendeleo,ilani na mapato na matumizi ,ina mapungufu makubwa.
Aidha madiwani hao wamewaagiza wataalamu na watendaji hao kufanya maboresho na kuirekebisha taarifa hiyo ili mwezi ujao iweze kujadiliwa na kupitishwa rasmi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti madiwani hao walisema,agenda ya kupitia taarifa hiyo muhimu ya uchaguzi ya mwaka 2015 wameiahirisha kwa ajili ya maboresho kabla ya kwenda chama.
Walielezea kuwa ni ngumu kuikwepa ilani ya chama tawala kwa kukubali kufanyakazi za serikali pasipo kuifanyia kazi ilani hiyo ambayo utekelezaji wake unakwenda sambamba na serikali iliyo madarakani.
 Diwani wa kata ya Visiga ,Mbegu Legeza,alisema watendaji ,wataalamu wa serikali sambamba na halmashauri wanapaswa kusimamia kikamilifu  utekelezaji wa ilani .
“Tuliyoyaona kwenye taarifa ya ilani hii mengi yamechotwachotwa na kubambikwa huku miradi mingine ikiwa haijawekwa kwenye taarifa hiyo”
“Mambo mengi hayapo sawa ukisema mmekopesha vikundi lazima iainishwe kata ngapi wamepewa hizo fedha,makundi gani yamepokea fedha,kuna viwanda vimejengwa na kuwekezwa vingine vimeandikwa vingine havijaandikwa”
“Kuna vikundi vimefundishwa lakini diwani wa kata husika hajui na kwenye kabrasha imeandikwa kuna elimu imetolewa kwenye kata hiyo hapo ni lazima diwani husika akatae”alisema legeza.
Diwani wa kata ya Mailmoja ,Ramadhani Lutambi alieleza kuwa ,hali hiyo inaonyesha udhaifu mkubwa kwa wataalamu hao kwa kushindwa kufanya kazi zao kwa uhakika.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Leonard Mloe,alikiri kuwepo kwa mapungufu kwenye taarifa hiyo ambapo alisema agenda nyingine zilijadiliwa na kupitishwa bila tatizo.
Agenda zilizojadiliwa ilikuwa ni pamoja na kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo robo ya nne april-juni  2016 ,taarifa ya maendeleo ya kata na kupokea taarifa ya mapato na matumizi.
Nae mwenyekiti wa CCM mji wa Kibaha ,Maulid Bundala, alitoa wito kwa baraza hilo kubadili utaratibu wa kupitia taarifa ya ilani kwenye baraza hilo kwa kutenganisha na kuichambua ilani hiyo kwenye vikao vingine ambavyo haviudhuliwi na viongozi wa vyama.
Alisema raha ya chakula usikione kikipikwa wala kuandaliwa hivyo ni vyema ukafanyika utaratibu mwingine wa kujadiliwa taarifa hiyo kwenye kikao cha madiwani pekee kabla ya baraza.
Hata hivyo Bundala alisema baada ya kujadiliwa taarifa hiyo ni lazima itafika katika chama hivyo hakuna sababu ya kujadiliwa wakati wao wakiwepo.
Alisema watendaji,watalaamu wa serikali na halmashauri hawawezi kukwepa ilani ya chama cha mapinduzi ,na kusema anaeona kichefuchefu kutekeleza ilani hiyo atoke nje wakati wa kuijadili.
“Itakuaje maziwa ya ng’ombe yawe mazuri halafu ng’ombe wake awe mbaya,serikali hii inaongozwa na CCM,sasa utakwepaje kuisimamia ilani ya chama tawala,jamani huu ni wakati wetu na ukifika wa chama kingine itasimamiwa ilani yao”alisema Bundala.
Bundala alieleza kuwa hata kama ni mkurugenzi ameajiliwa na serikali ambayo imenatekeleza ilani ya CCM hivyo kuna kila sababu ya watendaji wote kufanyakazi kwa moyo na kusimamia majukumu yao.
Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Kibaha ,Lucy Kimoi alisema wamepokea ushauri na maagizo yote na kuahidi kwenda kuyafanyia kazi.
Katika hatua nyingine halmashauri hiyo imekisia kukusanya kwa mwaka 2015/2016 bil 3.744 katika mapato yake ya ndani .
Robo ya nne inayoishia juni mwaka huu,imekusanya mil.732.102 na kufanya jumla ya mapato yaliyokusanywa julai /juni 2016 kuwa zaidi ya bil.2.910.866 sawa na asilimia 78 ya makisio.

Pia imekisia kutumia zaidi ya bil.31.836.942 kwa lengo la kutoa huduma kwa wananchi wa mji huo .
Katika utekelezaji wa shughuli zake kwa robo ya nne iliyoishia juni 2016 imetumia bil.5.950.420 na kufanya jumla ya matumizi kwa julai/juni  mwaka huu kufikia bil.21.614.164 sawa na asilimia 67 ya makisio.

No comments:

Post a Comment