Tuesday, 2 August 2016

MO DEWJI AMWAGA MILIONI 100 ZA USAJILI SIMBA SC JIJINI DAR LEO

Mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ameanza kuinufaisha klabu ya Simba baada ya kuipatia sh milioni 100 kwa ajili ya kusaidia zoezi la usajili. 

Dewji alikabidhi fedha hizo kwa Rais wa klabu ya Simba, Evans Aveva katika hafla fupi iliyofanyika makao makuu ya kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited zilizopo jengo la Golden Jubilee,jijini Dar. Akizungumza katika makabidhiano hayo, Dewji alisema kuwa fedha hizo ni mchango wake kwa timu hiyo ili kusajili wachezaji ambao imepanga kuwaongeza katika zoezi ambalo litaisha Agosti 6. 

Dewji alisema kuwa amefurahishwa sana na hatua ya uongozi na wanachama wa klabu hiyo kubariki mabadiliko ya uendeshaji na kuingia katika mfumo wa hisa. “Huu ni mchango wangu kama mwanachama wa klabu, nina mambo mengi mazuri yanakuja wakati wa kufanya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu,” alisema Dewji. 

“Simba SC ni timu kubwa sana, ina wanachama na mashabiki wengi, inahitaji kuwa na hadhi ya pekee kabisa, naamini kwa mchango huu, uongozi utaweza kumsajili mchezaji kutoka Ivory Coast ambaye kwa sasa anasubiri fedha ili aweze kusaini,” alisema. 

Rais wa Simba, Evans Aveva alimshukuru Dewji kwa msaada huo ambao utawawezesha kumsajili mchezaji, Frederick Blagnon. Alisema kuwa kwa sasa klabu yao inahitaji Sh milioni 320 ili kukamilisha usajili na kuwaomba wadau wengine kumuunga mkono Dewji. 

Mfanyabiashara maarufu nchini Mohamed Dewji akimkabidhi mfano wa hundi sh. milioni 100 Rais wa Simba SC, Evans Aveva kama mchango wake katika usajili wa klabu hiyo leo ofisini kwake,jijini Dar es salaam.
Mfanyabiashara maarufu nchini Mohamed Dewji a.k.a Mo Dewji akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari mapema leo jijini Dar,alipokuwa akikabidhi mfano wa hundi ya sh. milioni 100 kwa Rais wa simba sc,(pichani kushoto) Evans Aveva kama mchango wake katika usajili wa klabu hiyo.
Baadhi ya Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakisikiliza yaliyokuwa yakijiri ukumbini humo.

No comments:

Post a Comment