MUFTI wa Tanzania, Shehe Mkuu Abubakar Zubery (pichani), amesema Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) halitishwi na maneno yanayoendelea mitandaoni kuhusu kujengewa jengo katika Makao Makuu na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye ni Mkristo.
Mufti alisema kumekuwa na maneno mengi, yanayozungumzwa katika mitandao ya kijamii baada ya Makonda kusema atajenga jengo hilo katika makao makuu ya Bakwata, Kinondoni jijini humo, huko wengi wakisema kwa nini baraza hilo limekubali kujengewa na mtu ambaye sio Muislamu.
Alitoa kauli hiyo jana wakati Mkuu wa Mkoa huyo, akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo hilo ambalo litatumia Sh bilioni tano hadi kukamilika kwake.
Mufti Zubery alisema maneno hayo, hayawasumbui na wapo Wakristo wengi waliowahi kuchangia maendeleo kwa Waislamu, lakini hayakutokea maneno kama yanayotokea sasa.
“Kwa nini Rais wa Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa alipotupa Chuo Kikuu hamkusema? Wapo wadau wengi tu Wakristo walitoa… leo Makonda katoa maneno yamekuwa mengi.
Acheni jamani, mbona hayo ni maneno ya husda na choyo, Waislamu wametoa na sasa Wakristo. Hata Mtume amewahi kupokea misaada kama hiyo,” alisema Mufti.
Kwa upande wake, Makonda alisema hashangazwi na maneno yanayoendelea, kwani Watanzania wamekuwa wakibeza kila jambo zuri linalofanywa na viongozi. Alisema jengo hilo linatarajiwa kujengwa kwa udhamini wa Kampuni ya GSM Foundation, ambao walikubali kujenga kwa gharama zao mpaka kukamilika.
“Wengi waliuliza fedha nitatoa wapi, lakini wanasahau mimi ni mtu wa watu, nimezungumza na wadau wangu, wamekubali kujenga jengo hilo ambalo nimewataka wajenge kwa muda wa miezi kumi na nne,” alifafanua Makonda na kuwataka viongozi wa serikali kutoa kipaumbele kwa viongozi wa dini wanaotaka kupata huduma katika ofisi zao kwani ni watu muhimu na wanapaswa kuwa mbele wanapohitaji huduma.
No comments:
Post a Comment