Thursday, 12 May 2016

Chama cha Ushirika NANYUM Lindi chadaiwa milioni 433 na wakulima

Na Raymond Mushumbusi MAELEZO

Chama cha Ushirika (NANYUM) wilayani Lindi kitatakiwa kulipa deni la sh. milioni 433 kwa wakulima wa korosho wilayani humo baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa tukio la wizi wa fedha hizo lililodaiwa kufanyika Januari, mwaka huu.

Katika taarifa iliyotolewa leo (Mei 12,2016) na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi inasema kutokana na tukio lililotokea mnamo Januari 7, mwaka huu majira ya saa 12:30 za jioni huko kijiji cha Nambahu majambazi wapatao watatu wakiwa na bunduki huku wakitumia usafiri wa pikipiki walivamia Ofisi ya NANYUM na kupora pesa taslimu sh. milioni 433.

Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa siku ya tukio hilo, kiasi cha fedha hizo zilichukuliwa kutoka Benki ya  NMB ya Lindi Mjini zikisindikizwa na polisi hadi kijijini Nambahu wakiwa na viongozi wa chama hicho Bw. Mohamedi Chilumba na Bw.Hassani Mundedu na fedha hizo zilikabidhiwa na kupokelewa na chama kupitia vitabu vya mahesabu.

“Baada ya kupata taarifa ya tukio kutoka kituo cha polisi Tandahimba, polisi walikwenda kijiji hapo majira ya saa 4:30 usiku na kuchukua maelezo ya viongozi tisa wa NANYUM juu ya tukio hilo ambapo walitaka kupewa taarifa kama  kulisalia kiasi chochote cha fedha baada ya tukio.Lakini viongozi hao wote walikana kwamba hakuna hata kiasi kilichobakia” ilieleza taarifa hiyo.

Aidha taarifa hiyo ilifafanua kwamba katika uchunguzi wa polisi ulibaini kati ya sh. milioni 443 zilizokabidhiwa kwenye chama hicho kutoka benki ya NMB tawi la Lindi hazikuibiwa zote. Hivyo baada ya wajumbe wa bodi hiyo kuhojiwa na polisi jumla ya sh. milioni 32 zilipatikana.Hadi sasa baadhi ya wajumbe hao wanashikiliwa na polisi ili kubaini upotevu wa fedha hizo.

Taarifa hiyo ilieleza kwamba kama itathibitika kisheria kwamba viongozi wa chama hicho wamehusika katika tukio hilo na kupatikana na hatia ya wizi watalazimika kulipa fedha hizo na Serikali itaendelea kufuatilia matukio kama hayo na kuhakikisha kwamba wakulima wanapata haki zao.

No comments:

Post a Comment