Mbunge
wa Jimbo la Mpwapwa, Mhe. George Lubeleje akiwahutubia Wauguzi wa
Hospitali Teule ya Mvumi, Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma 14 Mei, 2016
wakati wa wakiadhimisha Siku ya Wauguzi Duniani.
Mkuu
wa Wilaya ya Chamwino, Mhe. Farida Mgomi (mwenye hijabu) akiwahutubia
Wauguzi wa Hospitali Teule ya Mvumi, Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma 14
Mei, 2016 wakati wa wakiadhimisha Siku ya Wauguzi Duniani.
………………………………………………………………………………..
Na Benedict Liwenga, MAELEZO, Dodoma.
Wauguzi Wilayani Chamwino pamoja
na wengineo nchini wamepewa pongezi kwa mchango wao mkubwa wanaoutoa wa
kutoa huduma ya afya kwa jamii ikiwemo kuendeleza huduma hiyo nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Mbunge
wa Jimbo la Mpwapwa, Mhe. George Lubeleje katika Hospitali Teule ya
Mvumi iliyopo Wilayani Chamwino mkoani Dodoma wakati alipomwakilisha
Spika wa Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai
ambaye alikuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi
Duniani.
Mhe. Lubeleje amesema kuwa bila
kuwepo kwa wauguzi huduma ya afya ingeyumba kutokana na ukweli kwamba
Wauguzi hao ni zaidi ya asilimia 60 ya Watumishi wote wa sekta ya afya
ambapo wanatekeleza asilimia 80 ya shughuli zote za afya.
Amefafanua kuwa, Wauguzi ndiyo
wenye kuandaa mazingira mazuri kwa daktari kutekeleza majukumu yake
kwani baada ya daktari kumaliza kumuona mgonjwa na kutoa maelekezo yake,
muuguzi husimamia utekelezaji wa maelekezo hayo pamoja na tiba na
huduma kwa mgonjwa husika.
Ameongeza kuwa, mara nyingi
muuguzi ndiye anayefanya kazi ya kuuguza mgonjwa kwani wagonjwa wengi
hutumia muda mwingi wakiwa mikononi mwa wauguzi kuliko wanaoutumia
mikononi mwa wahudumua wengine wa sekta ya afya.
Aidha, Mhe. Lubeleji amewapongeza wauguzi hao kutokana na kaulimbiu yao katika Maadhimisho ya Wauguzi Duniani isemayo “Wauguzi; Nguvu ya Mabadiliko: Uboreshaji wa uthabiti wa mifiumo ya afya”
ambapo amesema kwamba ni kaulimbiu katika wakati muafaka kwakuwa
wauguzi wana nafasi maalum katika maendeleo ya huduma ya afya na sekta
yenyewe kwa ujumla.
“Ni chachu muhimu ya mabadiliko
katika sekta ya afya, na ndiyo rasilimali ya kuwawezesha uboreshaji wa
uthabiti wa mifumo ya afya”, alisema Mhe. Lubeleje.
Akifafanua baadhi ya changamoto
zinazoikabili Hospitali Teule ya Mvumi wilayani hapo, alisema kuwa
Serikali inaelewa kuhusu mchango wa wauguzi na inauthamini kwa kiasi
kikubwa, vile vile amewahakikishia wauguzi hao kuwa Serikali imekuwa
ikijitahidi kuboresha maslahi ya Watumishi wa Umma wakiwemo wa afya,
hususani katika masuala ya mishahara na posho mbalimbali.
“Maombi yenu nimeyapokea na
ninaahidi nitayawasilisha kwenye Mamlaka husika kwa ajili ya
utekelezaji, yale yanayotuhusu, kama Bunge tutayachukua pia na
kuisimamia Serikali ili iyatekeleze na hatimaye tuimarishe huduma za
uuguzi na afya kwa ujumla”, alisema Mhe. Lubeleje.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya
Chamwino, Mhe. Farida Mgomi amewasisitiza Wauguzi wilayani hapo kujituma
kwa bidii katika kutekeleza majukumu yao ya kutoa huduma ya afya kwa
jamii kwani Serikali ya Awamu ya Tano inahitaji mabadiliko yanayoendana
na kasi ya “Hapa Kazi tu” kwa kuwahudumia wananchi nchini.
Aidha, amewapongeza kwa juhudi zao
na maarifa katika kazi yao na kuwahakikishia kuwa Serikali itazidi
kushirikiana nao katika kuleta maendeleo katika sekta hiyo na kusimamia
vema katika masuala yao mbalimbali.
Sikua ya Wauguzi Duniani
huadhimishwa tarehe 12 Mei kila mwaka ikiwa ni kumbukumbu ya kuzaliwa
kwa Mwanzilishi wa Uuguzi Bi. Florence Nightngale aliyezaliwa tarehe 12
Mei, 1820 na kufariki mwaka 1910.
No comments:
Post a Comment