Sunday, 15 May 2016

Majaliwa awapa mbinu Jumuiya
ya Madola kukomesha rushwa

Mwandishi Wetu, London

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Jumuiya ya Madola inaweza kuiga mbinu ambazo Tanzania imetumia katika kupambana na rushwa zikiwemo za kujumuisha wadau tofauti kwenye vita hiyo.

Ametoa kauli hiyo juzi, wakati akizungumza na Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo, Patricia Scotland walipokutana kwenye mkutano wa kimataifa uliojadili jinsi ya kupambana na rushwa duniani uliofanyika Lancaster House jijini London, Uingereza.

"Tanzania iko tayari kushirikiana na ninyi katika kujenga timu hii na ili uweze kupata picha halisi, nakukaribisha Tanzania uje ujionee hatua ambazo tumechukua hadi kufikia hapa tulipo kwenye vita hii dhidi ya rushwa," alisema  Majaliwa aliyehudhuria mkutano huo kwa niaba ya Rais John Magufuli.

Alimweleza Katibu Mkuu huyo kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kupambana na rushwa kutokana na ushirikiano mkubwa inaoupata kutoka kwa wananchi. "Wananchi wanafurahia juhudi za serikali, vyama vya kiraia pia vinaunga mkono jitihada zetu na vyombo vya habari vinashirikiana nasi katika vita hii," alisema.

Alitoa mwito huo baada ya kuelezwa na Scotland kwamba, anataka kuanzisha idara maalumu kwenye jumuiya hiyo itakayosimamia mapambano dhidi ya rushwa na makosa ya jinai.

"Nataka tuwe na idara yenye watu mahiri wa idara za uhasibu, mahakama yenyewe ikiwemo waendesha mashtaka na wanasheria kutoka kwenye nchi kadhaa ili washirikishane uzoefu kutoka kwenye nchi zao. Ninaamini katika nchi 53 ambazo ni wanachama wetu, sitakosa watu wa aina hii," alisema.

Alisema ameamua kufanya hivyo ili aweze kuendana na malengo makuu matatu ya jumuiya hiyo ambayo ni kupiga vita rushwa, kuhimiza utawala bora na usimamizi wa demokrasia.

No comments:

Post a Comment