Thursday, 12 May 2016

TANZANIA KUWA WENYEJI MKUTANO WA WAKADIRIAJI MAJENZI

indexNa Beatrice Lyimo-MAELEZO DAR ES SALAAM.
…………………………………………………
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano mkuu wa wakadiriaji majenzi Afrika unaotarajiwa kufanyika tarehe 18-19 Agosti, 2016 jijini Dar es salaam.
Hayo yamesemwa leo na Rais wa chama cha wakadiriaji majenzi Tanzania (TIQS) Samuel Marwa kuwa Tanzania kwa mara ya kwanza imekuwa mwenyeji katika mkutano huo ukiwa na lengo la kukuza fani ya ukadiriaji majenzi ili mchango wake katika jamii uweze kutambulika.
Amesema mada kuu ya mkutano huo ni kufikia malengo ya maendeleo endelevu na mchango wa huduma za ukadiriaji majenzi hivyo sekta ya ujenzi na hasa miundombinu ni moja ya vipaumbele vilivyoainishwa kama kichocheo cha kuwezesha kufikia malengo ya maendeleo endelevu na kukuza uchumi wa nchi.
“Malengo ya Maendeleo Endelevu yanakusudia kuondoa umaskini na kupambana na udhalimu na kuleta usawa pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi kufikia mwaka 2030, hivyo mada hii inaendana na na jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuleta maendeleo yenye usawa, mafanikio na ustawi wa kila mwananchi”alifafanua Rais huyo.
Aidha, amesema kuwa  huduma hizo, zikitumika kwa ukamilifu zitasaidia kupambana na rushwa na uwajibikaji dhaifu kwani huduma hiyo ni nguzo muhimu katika kuchangia ufanisi na udhibiti wa gharama za ujenzi  na ukamilishaji kwa muda wa  miradi na kupata dhamani ya fedha.
Mbali na hayo Rais huyo ameuomba uongozi wa vyuo tofauti nchini kuanzisha na kuzidi kudahili wanafunzi katika taaluma ya ukadiriaji majenzi ili kutatua changamoto zilizopo.
Nchi zaidi ya 16 za Afrika zilizoko Jumuiya ya Madola pamoja na Angola na Msumbiji  zinatarajiwa kushiriki katika mkutano huo.

No comments:

Post a Comment