Thursday, 26 May 2016

TANZANIA YAPIGA HATUA KUBWA KATIKA MATUMIZI YA HUDUMA ZA MITANDAO



Na Jacquiline Mrisho- MAELEZO

Tanzania imepiga hatua kubwa sana katika sekta ya mawasiliano  hadi kufikia kuwa kwenye kundi la  nchi zilizoendelea kimawasiliano Duniani.

Takwimu zinaonyesha kuwa watanzania takribani milioni 39 wana laini za simu za kiganjani pamoja na watumiaji wa intaneti takribani milioni 20 ambapo miaka ya nyuma idadi ya laini za simu za kiganjani zilikuwa 2,963,737.

Haya ni maendeleo makubwa yanayoifanya Tanzania kuwa nchi bora kwa upande wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi James Kilaba alisikika akisema kwamba,"Ukuaji wa kasi wa sekta ya mawasiliano nchini umechangia sio tu katika kuboresha maisha ya wananchi kijamii na kiuchumi bali unachangia sana katika kuinua pato la Taifa".

Ukuaji huu umetokana na kuwepo kwa sera, sheria, kanuni na mfumo mzuri wa utoaji leseni za huduma za mawasiliano.

Kama wasemavyo wahenga kuwa ya Kaisari tumpe Kaisari basi sifa zote ziwaendee Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kwa kazi nzuri wanazozifanya.

TCRA wana jukumu la kusimamia shughuli  hizo zote wakishirikiana na wadau wa mawasiliano nchini katika kusimamia na kuzitekeleza kwa makini sera,sheria na kanuni hizo ili kuwezesha kupatikana kwa huduma za mawasiliano nchini kote kwa kushawishi uwekezaji ,kusimamia vizuri ushindani pamoja na kutoa fursa sawa kwa watoa huduma.

TCRA inaendelea kuhakikisha kuwa rasilimali adimu zikiwemo za masafa na namba za simu zinatumika kwa makini ili kukidhi mahitaji ya Taifa na maendeleo ikiwa ni kutekeleza lengo la Serikali la kuwawezesha wananchi wote kupata habari na kuhakikisha hawaachwi nyuma katika maendeleo ndani ya karne hii ya utandawazi.

Huduma hizi za mitandao pia zimegawanyika kutokana na kutofautiana kwa mahitaji ya wananchi. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania,  huduma za mitandao ni kama ifuatavyo; Intaneti, Benki Mtandao, Elimu Mtandao, Matibabu Mtandao,Biashara Mtandao, Malipo Mtandao pamoja na Mawasiliano Mtandao.

Huduma hizi zimekuwa zikirahisisha mambo mengi hasa ya kikazi na ya kijamii,ukiangalia kwa sasa ofisi zote za umma na za binafsi wanatumia huduma za mitandao katika kufanya shughuli zao zote za kiofisi kama njia salama ya kuhifadhi data zao.

Kwa ofisi za  Serikalini wameipa huduma hii jina la Serikali Mtandao (E-Government) ambapo watumishi wa umma wanashauriwa kutumia mtandao huu ili kuhakikisha kazi zote za ofisi zinafanyika katika hali ya usalama na usiri mkubwa.

No comments:

Post a Comment