Thursday, 12 May 2016

WAKAZI WA VIJIJI VITANO WATOA MAONI YAO UENDESHAJI SERA YA ARDHI



WAKAZI WA VIJIJI VITANO WATOA MAONI YAO UENDESHAJI SERA YA ARDHI

24news.blogspot.com, Mwanza

Wakazi wa vijiji vitano vya Nyanguge, Ihayabuyaga, Muda, Matela na Bugumangala Wilaya ya Magu mkoani Mwanza wametoa maoni yao kuhusu uboreshaji wa Sera ya Ardhi ya mwaka 1995 ili kukidhi mahitaji ya sasa.

Akitoa mada kabla ya wananchi hao kutoa maoni Mwezeshaji wa Kitaifa Sera ya Taifa ya Ardhi Dk. Medard Geho alisema watafakari kwa kina ili sera itakayotengenezwa iwe kwa ajili yao na vizazi vyao na hivyo kuiwezesha sekta ya ardhi kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa Watanzania.

“Serikali imeagiza sera hiyo ipitiwe upya kulingana na mabadiliko ya kiuchumi na uwekezaji na hivyo tuwe na fikra mpya ili ardhi itukumboe  kiuchumi na kuleta maendeleo ya kiuchumi na tuondokane na umasikini na hatuwezi kuondoa umasikini kwa kumiliki mashamba madogo madogo,”alisema Dk.Geho.

Naye Kamishna msaidizi wa Ardhia Kanda ya Ziwa Joseph Shewiyo Ziwa, alisema kuwa kupitia upya sera na matamko yake na sheria hiyo ya ardhi umelenga kuondoa tunayoona hayatusaidii na jambo gani liingizwe kwenye sera na kutungiwa sheria kulinga na mabadiliko ya kiuchumi na kuongezeka kwa idadi ya watu na mifugo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Matela Joseph Maneno alipendekeza mfumo wa umiliki ardhi ushuke kutoka miaka 93 hadi 30 kwa wawekezaji,mikataba ya uwekezaji vijijini ifungwe na serikali za vijiji badala ya halmashauri na wizara.

Naye Afisa Tarafa Kahangara Thomas Makobela alipendekeza ili kuongeza ukubwa wa mabaraza ya kushughulikia migogoro ya ardhi kwa kuingiza makundi maalumu , serikali za vijiji zipewe hati miliki ya ardhi zitumike kukopa kwenye taasisi za fedha na mabaraza hayo yaendeshwe bila gharama za fedha.

Aidha, wananchi hao walipendekeza hati miliki za ardhi zitolewe wilayani badala ya wizara na utaratibu wa utoaji hati za kimila na za serikali uendelee kama ulivyo na fidia ya ardhi ilipwe kwa mmiliki mwenyewe kukubaliana na kiwango badala ya fidia kulipwa na halmashauri.

Walisema ili kuondoa migogoro kati ya wakulima na wafugaji maeneo yao yatengwe na yenye madini wamiliki waingie ubia na kuwe na sera ya umbali wa kuchimba wa mita 50 kwenda chini.

Pia walipendekeza watumishi wa ardhi wahamishiwe wizara husika, maeneo ya makazi, kilimo,mapotri ya akiba na hifadhi  na wafugaji yatenganishwe,kila baada ya miaka 20 serikali iwe na mkakati maalumu wa kupima ardhi kwa matumizi ya baadaye.

Mjumbe wa baraza la ardhi la Kijiji cha Ihayabuyaga Winga Joseph aliomba yapewe vitendea kazi, uwezeshaji (posho) hati za ardhi zitolewe  vijijini ili kuwaondolea kero ya kuzifuata wizarani.

Mwisho

No comments:

Post a Comment