Tuesday, 24 May 2016

TAASISI YA MBALAWALA YAIPONGEZA NISHATI NA MADINI KUWEZESHA SHUGHULI ZAKE KUFAHAMIKA

Meneja Uendeshaji kutoka Taasisi ya Wanawake ya Mbalawala Women Organization inayojishughulisha na uzalishaji wa briketi za makaa ya mawe wilayani Mbinga mkoani Ruvuma, Hajiri Kapinga (kulia) akielezea mafanikio ya taasisi hiyo mara baada ya taarifa zake kuanza kuchapishwa katika Jarida la Wizara. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasilano Serikalini Wizara ya Nishati na Madini, Asteria Muhozya.

Na Greyson Mwase, Dar es Salaam

Taasisi ya Wanawake ya Mbalawala inayojishughulisha na uzalishaji wa braketi za makaa ya mawe ijulikanayo kama Mbalawala Women Organization yanye makazi yake katika kijiji cha Ruanda wilayani Mbinga mkoani Ruvuma imeipongeza Wizara ya Nishati na Madini kupitia Kitengo cha Mawasiliano Serikali kwa kutangaza shughuli zake hali iliyopelekea wateja wa makaa ya mawe katika taasisi hiyo kuongezeka kadri siku zinazokwenda.

Taasisi hiyo inayofanya shughuli zake karibu na Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Ngaka inajishughulisha na utengenezaji wa briketi bora za makaa ya mawe kwa ajili ya kupikia

Pongezi hizo zilitolewa na Meneja Uendeshaji wa Taasisi hiyo Hajiri Kapinga aliyekutana na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasilano Serikalini Wizara ya Nishati na Madini, Asteria Muhozya jijini Dar es Salaam na kusema kuwa tangu Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kianze kuchapisha habari zinazohusu taasisi hiyo kupitia Jarida lake linalochapishwa kila wiki lijulikanano kama MEM Newsbulletin wameshuhudia idadi kubwa ya wateja ikiongezeka na kuzidi uzalishaji wa taasisi hiyo.

Alisema kabla ya habari zake kuchapishwa na Jarida la Wizara, taasisi hiyo ilikuwa ikiwauzia briketi za makaa ya mawe wateja wake walioko katika vijiji vinavyozunguka mgodi wao wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.

“Mara baada ya taarifa zetu kuanza kuchapishwa na Jarida la Wizara ya Nishati na Madini tumeshuhudia mabadiliko makubwa kwani tumekuwa tukipokea simu kutoka mikoa mbalimbali hususan Dar es Salaam, Mbeya, Iringa wateja wakihitaji bidhaa, hali inayopelekea mahitaji kuwa makubwa kuliko kiasi tunachozalisha,.” alisema Kapinga.

No comments:

Post a Comment