Hussein Makame-MAELEZO
………………………………………..
Wakati dunia ikiadhimisha siku ya
mama, heshima, thamani na nafasi ya mama imeanza kupotea kwa siku za
karibuni kwani mama anadhalilishwa na wengine kuthubutu kumwambia “kama
ungelichelewa kunizaa ningelikuzaa wewe”.
Mama ni kiumbe aliyepewa nafasi
kubwa katika familia na jamii kwa ujumla. Hii inathibitishwa na thamani
ambayo Mungu amempa mama kutokana na majukumu yake katika kujenga
familia na jamii bora.
Mafanikio ya jamii yanategemea kwa
kiasi kikubwa mchango wa mama na pindi anaposhindwa kutekeleza majukumu
yake huweza kusababisha familia na jamii mzima kuharibikiwa.
Hata hivyo ili mchango wa mama
katika familia na jamii uonekane ni lazima watoto na jamii inayomzunguka
imuheshimu, imjali na kumthamini na kumpa huduma zinazotakiwa.
Heshima ya pekee ambayo mama
anastahili kuipata kutoka kwa mtoto na jamii ni kufuata yale mazuri
anayoelekeza na kuacha kufanya yale ambayo anayachukia wakati anapomuona
mtoto au mwanajamii anayafanya.
Pia mama anastahili kuthaminiwa
kwa kumsaidia shida zake pale anapohitaji msaada na kuhakikisha nafasi
yake akiwa mlezi inazingatiwa kwa uzito unaostahili.
Nafasi ya mama kwa mtoto na jamii
ni kumfanya kuwa kiongozi, mwamuzi na mshauri pale mtoto au jamii
inapohitaji kuongozwa au kushauriwa katika mambo yenye maslahi kwa mtoto
na jamii yake.
Na pale mtoto anapokosea ni vyema akawa tayari kusikiliza mwongozo mzuri anaopewa na mama na kuwa tayari kurekebishika.
Tumezoea kusikia siku hizi wazazi
wengi wakilalamika kwamba “mtoto huyu siku hizi amenishinda”. Hii ni kwa
sababu watoto wengi hawawatii wazazi na mama zao matokeo yake
wanaharibikiwa kimaisha na kujiingiza kwenye makundi mabaya.
Wakati upande mmoja ukionesha
jinsi mama anavyokosa heshima, thamani na nafasi yake kutopewa uzito
katika familia, kwa upande wa pili tunao baadhi ya kina mama hawafai
hata kuitwa mama.
Hii ni kwa sababu ya matendo
wanayoyafanya ambayo hayaoneshi heshima, thamani na nafasi yao katika
familia kwani hatutegemei mama asiyejiheshimu akawa mlezi wa familia
maana kulea ni kuongoza njia.
Kuongoza njia ni kuonesha mfano
mzuri lakini kuna baadhi ya kinamama matendo yao yanaongoza njia ambayo
hata shetani anaogopa kupita, matokeo yake anakuwa chanzo cha kuiharibu
familia na jamii.
Baadhi ya kina mama wamekuwa na
tabia chafu na mbaya zisizostahili kuigwa katika jamii kuanzia muonekano
wao, mambo wanayofanya, mavazi yao na maisha wanayoishi.
Wengine wanafanya biashara ya
kuuza miili yao bila kujali ubaya na hatari inayowakabili.Wengine
huwachukua mabinti wadogo kutoka mikoani na kuwafanyisha biashara chafu
kwa wanaume.
Katoto na jamii inayomzunguka
inajifunza nini kutoka kwa mama kama huyo. Hii si sawa kabisa na
tunapoadhinisha siku hii ya mama ni lazima akina mama wa aina hii
wajitafakari na kujirekebisha mara moja.
Tunapoadhimisha siku ya mama
duniani kila mama anahitaji kujiuliza ni mama wa aina gani na anafanya
nini kutekeleza jukumu kubwa katika kujenga familia yake na jamii bora.
Hatuwezi kuwa na jamii
iliyoendelea na inayozingatia malezi bora ya watoto na jamii kwa ujumla,
bila kuwa na mama anayejitambua heshima yake, thamani na nafasi yake.
Jamii haiwezi kuepuka watoto
wanaoishi kwenye mazingira magumu, hatuwezi kuepuka maradhi na
udhalilishaji wa watoto na kuwa na jamii yenye maambukizi sifuri ya HIV,
bila ya kuwa na mama anayethamini utu.
Hivyo ni imani yangu kuwa siku hii
haitatufanya kuwakumbuka mama zetu na kushiriki nao kwenye majukwaa na
maeneo ya furaha, bila kuzingatia na kuhakikisha mama anapewa heshima
yake na anathaminiwa na jamii.
Ni vyema tukajadili haya kwa
sababu binadamu siku zote hubadilika na asipokumbushwa anaweza kupotea
njia na kibaya zaidi anaweza kuipoteza familia na jamii kwa ujumla na
tukavuna majuto.
Ni bahati mbaya iliyoje siku ya
mama duniani kupita hivihivi bila kusikia jamii ikijumuika pamoja na
kutafakari nafasi ya mama na changamoto zinazomkabili mama katika
kufikia malengo ya kujenga jamii iliyo bora.
Binadamu siku zote ana tabia ya
kubadilika na asipokumbushwa anaweza kupotea njia na kibaya zaidi
anaweza kuipoteza familia na jamii kwa ujumla kutokana na matendo yake.
Wakati tukiathimisha siku ya mama
ni vyema tukatafakari kwa pamoja tukizingatia kwamba kwenye msafara wa
mambo hata kenge wamo na tukiwaachia kenge wakatawala msafara huu
tutakuwa tunasherehekea kuharibika kwa familia na jamii yetu.
Thamani ya mwanadamu imetokana na
jinsi Mungu alivyomuumba kuwa bora kuliko viumbe wengine maana amepewa
akili ya kutambua zuri na baya na kutakiwa kuishi kwa kufanya mazuri na
kuacha kutenda mabaya.
Heshima na thamani yake itaendelea
kubaki kutokana na jinsi anavyoitumia akili yake kutafakari anayofanya
na hapo atakuwa amethamini nafasi aliyotunukiwa na Mungu na kubithibisha
ubora wake.
Ni vyema tukayazingatie haya kwa
heshima, thamani na nafasi ya mama katika familia na jamii yetu la sivyo
tutakuwa tujiunguza kwa mikono yetu huku tukisherehekea.
Maoni:0766496589
No comments:
Post a Comment