Na Takdir Ali-Maelezo Zanzibar .
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema haitamvumilia mfanyabiashara yeyote atakayebainika kuuza bidhaa zilizopitwa na wakati.
Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Balozi Amina Salum Ali, amesema kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi juu ya tabia ya baadhi ya afanyabiashara kuwauzia vitu vilivyopitwa na wakati.
Amefahamisha kuwa, udanganyifu huo unaofanywa na wafanyabiashara huwasababishia wananchi kupata maradhi mbalimbali ikiwemo saratani.Akiwa katika ziara ya kukagua maghala mbalimbali ya chakula kisiwani Unguja kuelekea mwezi mtukufu wa Ramadhani, Balozi Amina amesema serikali imechoka kuona wananchi wanauziwa vyakula visivyokuwa na kiwango kutokana na kumalizika muda wao wa matumizi.
Waziri huyo amekemea vitendo vya baadhi ya wafanyabiashara kuuza vyakula vilivyokaa maghalani kwa muda mrefu hata kupindukia miaka mitano, hali aliyosema ni kuwaathiri na kuwadhulumu wananchi.“Wazanzibari tumechoka kulishwa michele mibovu. Tunasema sasa imetosha na hatutawafumbia macho wafanyabiashara watakaoendeleza vitendo hivyo,” alisema Waziri Amina.
Amesema serikali inakusudia kuweka bei elekezi kwa wafanyabiashara wote ili kuzuia upandaji bei kiholela hali inayowapa usumbufu wananchi hasa wa kipato cha chini.Aidha Balozi Amina amesema kila mwaka ifikapo mwezi mtukufu wa Ramadhani, serikali imekuwa ikipunguza kodi za bidhaa muhimu kwa wafanyabiashara ili kutoa punguzo kwa wananchi.
Amezitaja bidhaa hizo kuwa ni unga wa ngano, sukari na mchele.
Hata hivyo, ameeleza kusikitishwa kwake kwamba bei za bidhaa hizo zimebakia palepale au kuongezeka zaidi licha ya nia nzuri ya serikali.Ili kuandaa mazingira ya kuwapa unafuu wananchi, amesema serikali inakusudia kukaa na wafanyabiashara wote ili kujadili na kupanga mipango mizuri kwa itakayowaletea maendeleo wafanyabiashara hao na taifa kwa jumla.
Kwa upande wao, wafanyabiashara waliotembelewa na Waziri huyo, wamemuhakikishia kuwa chakula kipo cha kutosha katika kipindi hiki cha kuelelekea mwezi mtukufu wa Ramadhani.Aidha wamesema chakula hicho kimeagizwa miezi mitatu kabla ya mwezi huo.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mfanyabiashara Abdulghafar Ismail Mohammed wa kampuni ya Evergreen Ltd, ameiomba serikali kukaa pamoja nao pale inapotaka kufanya maamuzi yoyote yanayowahusu ili kuweka uwiano kwa upande wao, serikali na wananchi.
Ziara ya Balozi Amina ilihusisha maghala ya kampuni za Yassir Provision, Akhtar Enterprises Malindi, Evergreen Ltd Saateni, Sub Sahara Maruhubi, Azam Mtoni, Vigor Turkey Group na Bopar Enterprises zote za Mombasa mjini Unguja.
Pamoja na kujua akiba ya chakula iliyopo nchini kupitia ziara hiyo, Waziri Amina pia alitaka kujua hali ya mfumko wa bei kuelekea mwezi mtukufu wa Ramadhani unaotarajiwa kuanza mwanzoni mwa wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment