Tuesday, 7 June 2016

SERIKALI YASEMA KISIWA CHA SHUNGIMBILI KILICHOPO WILAYA YA MAFIA, PWANI HAKIJAUZWA



Na Ismail Ngayonga-MAELEZO

SERIKALI imesema kisiwa cha shungimbili kilichopo Wilayani Mafia mkoani Pwani hakijauzwa kwa kampuni ya Zululand ya Afrika Kusini na badala yake kimeingizwa katika uwekezaji kupitia kampuni ya Thanda Tanzania Ltd inayojenga hoteli ya kitalii.

Akijibu swali la Mbunge wa Mwanakwerekwe (CCM), Ali Said Khamis, leo Bungeni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani alisema Alisema uwekezaji huo umepitia taratibu zote za Serikali na pindi utakapokamilika mwekezaji atatekeleza wajibu wake ikiwemo kulipia tozo zote kwa mamlaka zinazohusika kwa mujibu wa sheria.

Makani alisema alisema kisiwa cha shungimbili ni miongoni mwa visiwa 15 ambayo ni maeneo tengefu yanayosimamiwa na Taasisi ya Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu nchini (MPRU).

Mhandisi Makani alisema MPRU iliianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Bunge na.29 ya mwaka 1994 ambapo miongoni mwa majukumu yake ni kusimamia maeneo yote yaliyotangazwa kuwa hifadhi za Bahari na maeneo tengefu ya bahari.

Aliongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa ndiyo yenye dhamana ya kuingia mikataba  yote ya kimataifa yenye maslahi kwa Taifa.

Aidha akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Singida, Martha Mlatta, Makani alisema Serikali inaendelea kuvijengea uwezo vyuo vya utalii vilivyopo nchini ili kuhakikisha kuwa wahitimu wake wanakuwa mahiri katika soko la ajira nchini.

“Mfanyabiashara akitafuta mwajiriwa ni lazima ahakikishe kuwa anaye mwajiri anakuwa na sifa zote za kumletea faida, hivyo na sisi pia tunataka wahitimu wetu katika vyuo vya utalii wanakuwa wanapata umahiri wa kutosha ili waweze kuajiriwa katika nafasi za juu kabisa katika kampuni yoyote”   alisema Makani.

Mbunge Mlatta alitaka swali lake la nyongeza alitaka kufahamu Serikali ina mikakati ipi katika kuhakikisha kuwa wahitimu wa Tanzania wanapewa nafasi za juu za kazi katika hoteli za kimataifa.

No comments:

Post a Comment