Thursday, 16 June 2016

KAMPUNI YA ASAS DAIRIES LTD YASHINDA TENA TUZO YA UBORA




Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Mary Mashingo akimkabidhi meneja uzalishaji wa kampuni ya Asas Dairies Ltd Bw Lipita Mtimila tuzo baada ya kampuni yake kushinda tuzo ya ubora katika maonyesho ya wiki ya Maziwa Nchini 
Tuzo ya Ushindi ya mwaka 2016
KAMPUNI ya Asas Dairies Ltd ya mkoani Iringa kwa mara ya nne mfululizo imeendelea kushika nafasi ya kwanza kitaifa uzalishaji wa maziwa nchini . Kampuni hiyo imeshinda tuzo ya wazalishaji wakubwa wa bidhaa bora za maziwa katika mashindano wiki ya maziwa yaliyofanyika juzi kwenye viwanja vya shule ya sekondari Mpechi mkoani Njombe .

Kampuni hiyo imeibuka mshindi wa kwanza baada ya kuongoza katika nafasi zote tatu za ubora wa bidhaa zilizoshindanishwa katika mashindano hayo .Akikabidhi tuzo hizo Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Mary Mashingo pamoja na kupongeza makampuni yaliyoshiriki katika zoezi hilo bado alipongeza kampuni ya Asas Dairies Ltd kwa kufanya vizuri katika mashindano hayo ya ubora wa maziwa nchini

Alisema kuwa jitihada zilizoonyeshwa na kampuni hiyo ni kubwa na zinapaswa kuigwa na makampuni mengine hapa nchini.Kwani alisema kuwa kuongoza katika nafasi zote zilizoshindaniwa si jambo dogo ni jitihada kubwa zimefanyika na ni hatua ya kujivunia kwa kampuni hiyo.

Pia aliipongeza bodi ya maziwa Tanzania kwa kuandaa mashindano kama hayo kwani ni sehemu ya kipimo kwa wamiliki wa viwanda vya maziwa nchini na sehemu ya kujitathimini . Kwa upande wake meneja uzalishaji wa kampuni hiyo ya Asas Dairies Ltd Lipita Mtimila alisema kuwa mbali ya kampuni hiyo kuongoza kwa mwaka huu bado ilipata kuongoza katika mashinadano kama haya miaka mitatu nyuma na hii ni mara ya nne kuongoza .

Katika mashindano hayo yaliyoandaliwa na bodi ya maziwa Tanzania( TDB) kampuni ya Asas Dairies iliweza kuibuka na ushindi wa jumla baada ya kushinda tuzo zote tatu dhidi ya makapuni mengine ya uzalishaji maziwa yaliyoshiriki katika mashindano hayo .Bw Mtimila aliwataka watanzania kuendelea kuzipenda bidhaa za Asas Dairies Ltd na kuwa lengo la kampuni hiyo ni kuendelea kuzalishaji bidhaa zenye ubora zaidi .Pia alipongeza watanzania na watumiaji wa bidhaa za Asas Dairies Ltd kutokana na ushirikiano mkubwa wanaoutoa kwa kuendelea kutumia maziwa yanayozalishwa na kampuni hiyo ya Asas Dairies Ltd Iringa
 Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Mary Mashingo akitembelea banda la kampuni ya Asas dairies Ltd 

No comments:

Post a Comment