Tuesday, 7 June 2016

WANANCHI WATAHADHARISHWA KUHUSU MABADILIKO YA HALI YA HEWA.



Meneja wa Kituo Cha Utabiri Kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Bw. Samwel Mbuya akizungumza na Waandishi wa Habari Leo Jijini Dar es salaam kuhusu mwelekeo wa Hali ya joto na mvua katika kipindi cha juni hadi Agosti 2016 ambapo inatarajiwa kuwa na hali ya baridi kiasi na vipindi vifupi vya mvua. Kulia ni Afisa Uhusiano wa Mamlaka hiyo Bi Monica Mutoni
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)na vyombo vya Habari Leo Jijini Dar es salaam.(Picha na Maelezo).

MAMLAKA YA HALI YA HEWA (TMA) YATOA MWELEKEO WA HALI YA HEWA KWA KIPINDI CHA JUNI HADI AGOSTI 2016.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa mwelekeo wa hali ya hewa kwa kipindi cha Juni hadi Agosti mwaka huu. Akizungumzia kuhusiana na mwelekeo huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Meneja Kituo Kikuu cha Utabiri Bw. Samwel Mbuya alisema “Nchi yetu inatarajia kuwa na hali ya baridi kiasi katika kipindi hiki sambamba na vipindi vifupi vya mvua vinavyotarajiwa kujitokeza katika maeneo machache hususanya ukanda wa Ziwa Viktoria na ukanda wa pwani ya Kaskazini (Visiwa vya Unguja na Pemba).

Katika kipindi cha mwezi Juni hadi Agosti 2016, maeneo mengi ya nchi yanarajiwa kuwa makavu na yenye hali ya baridi kiasi katika majira haya ya kipupwe. Mifumo ya hali ya hewa inaonesha matarajio ya hali ya joto la wastani hadi chini ya wastani katika maeneo yaliyopo Kusini-magharibi mwa nchi. 

Hata hivyo,katika msimu wa Kipupwe wa mwaka huu maeneo mengi ya nchi yanatarajiwa kuwa na joto la wastani hadi juu ya wastani. Aidha, izingatiwe kuwa hali ya ubaridi inatarajiwa zaidi nyakati za usiku hadi mapema asubuhi. “Aliendelea kueleza sababu za hali hiyo kuwa ni pamoja na kupungua kwa joto la bahari katika eneo la ukanda wa Tropiki la bahari ya Pasifiki sambamba na Joto la baharí katikaeneo la magharibi wa bahari ya Hindi kuwa la wastani kwa kipindi cha miezi ya Juni hadi Agosti 2016”. 

Aidha, joto katika bahari ya Atlantiki linatarajiwa kuwa chini ya wastani. Hali hiyo inatarajiwa kusababisha upepo kuvuma kutoka magharibi ukielekea mashariki hususankatika maeneo ya Ukanda wa Ziwa Viktoria. Joto la bahari la juu ya wastani linatarajiwa katika eneo la ncha ya kusini ya bara la Afrika hivyo kuathiri msukumo wa upepo wa kusi.

Kwa upande mwengine, Afisa Uhusiano wa TMA, Bi. Monica Mutoni alitoa msisitizo kwa wananchi kufuatilia taarifa hususan za tahadhari zinazotolewa na Mamlaka kupitia vyombo mbalimbali vya habari, tovuti ya Mamlaka n.k ili kuokoa maisha na mali. Bi. Monica alisema “Hivi karibuni TMA imekuwa ikitoa tahadhari mbalimbali ikiwa ni pamoja na za kuwepo kwa upepo mkali na mawimbi makubwa kwenye ukanda wa Bahari Hindi, Maziwa na nchi kavu hivyo ni vyema wananchi hasa wale watumiaji wa bahari na maziwa kuchukua hatua stahiki pindi taarifa kama hizo zinapotolewa”.

Aidha, TMA ilipongeza sekta mbalimbalipamoja na Taasisi, Mamlaka za Serikali na jamii kwa ujumla kwa hatua stahiki zilizochukuliwa katika kipindi chamsimu wa mvua za Masika 2016 kwa kutumia Taarifa, Agalizona Tahadhari za utabiri zilizotolewa na Mamlaka. Ni wazi kuwa kwa hatua hizo madhara ambayo yangeweza kujitokeza yalidhibitiwa na hivyo kuchangia katika kufanikisha mipango na utekelezaji wa shuguli za kiuchumi na kijamii katika kipindi husika.

Kwa tarifa ya kina kuhusiana na mwelekeo wa hali ya hewa kwa mkoa wako ingia kwenye tovuti ya TMA www.meteo.go.tz au tembelea ofisi zetu

IMETOLEWA NA MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

No comments:

Post a Comment