Thursday, 16 June 2016

KAPOMBE AWA MCHEZAJI BORA WA MSIMU WA AZAM




Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii

BEKI mahiri wa kulia wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Shomari Kapombe, amechaguliwa na mashabiki kuwa Mchezaji Bora wa timu hiyo msimu uliopita ambalo zoezi hilo la kumtafuta mchezaji wa kutwaa tuzo hiyo lilianza rasmi Juni 8 mwaka huu kwa hatua ya awali kabla ya Ijumaa iliyopita kuingia hatua ya fainali iliyohusisha wachezaji sita waliopigiwa kura nyingi zaidi na mashabiki katika akaunti ya Azam FC kwenye mtandao wa kijamii wa facebook.

Hadi zoezi hilo linafikia tamati Kapombe ameweza kuwabwaga wapinzani wenzake watano kwenye kinyang’anyiro hicho ambao ni Nahodha Msaidizi Himid Mao ‘Ninja’, beki kisiki Pascal Wawa, kipa Aishi Manula na mawinga Farid Mussa na Ramadhan Singano ‘Messi’. Beki huyo ametwaa tuzo hiyo baada ya kujizolea kura 203 kati ya zote 560 zilizokubaliwa, Aishi amemfuatia akiwa nazo 125, Farid (95), Singano (48), Himid (45) na Wawa (44).

Mashabiki wengi waliompigia kura Kapombe hawakusita kufanya hivyo wakidai alikuwa ni nguzo muhimu kwa Azam FC msimu uliopita baada ya kucheza kwa bidii na kufunga mabao muhimu kwa timu hiyo na hata alipokosekana pengo lake lilionekana huku pia wengine wakimpongeza Aishi Manula aliyeshika nafasi ya pili wakisema naye alifanya kazi kubwa.

Mbali na tuzo hiyo ya mashabiki, Kapombe pia alifanikiwa kuwa mchezaji pekee wa Azam FC aliyepata Tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi inayotolewa na mdhamini wa Ligi Kuu, Kampuni ya Vodacom, akitwaa ya mwezi Januari mwaka huu na moja ya rekodi zake za msimu uliopita, ni kuwa beki pekee wa ligi hiyo aliyefunga mabao mengi kuliko mwingine yoyote akitupiwa wavuni mabao nane huku katika mechi zote ilizocheza Azam FC akicheka na nyavu mara 12 na kutoa pasi za mwisho saba na akicheza jumla ya dakika 3188.

No comments:

Post a Comment