Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Muziki Tanzania John Kitime anatarajia kuunda Chama kwa ajili ya waandishi wa habari wanaoandika habari za wanamuziki ili waweze kupeleka taarifa sahihi za wanamuziki kwa wananchi.
Akiongea na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Katibu huyo amesema kuwa kuunda chama hicho ni moja ya matarajio yake anayopanga kulifanyia shirikisho hilo.
“Kati ya vitu nilivyovipanga kuvifanya katika shirikisho hili, ninatarajia kuhamasisha uundaji wa chama cha waandishi wanaoandika habari za wanamuziki ili waweze kufanya kazi kwa pamoja ya kupeleka taarifa sahihi za wanamuziki kwa wananchi”, alisema Kitime.
Kitime ameongeza kuwa matarajio yake mengine anayotarajia kuyafanya ni kutoa elimu kwa wanamuziki kuhusu kazi zao kupitia semina mbalimbali pamoja na kuimarisha shirikisho hilo ili wanamuziki waweze kusimama, kukuza muziki pamoja na kunufaishwa na muziki.
Aidha, ameelezea kuwa vyama 8 ambavyo tayari vipo katika shirikisho hilo vitasaidiwa ili kuwa na nguvu ya kuweza kusimama na kuwasaidia wanamuziki inavyostahili kwa kuwa nia na madhumuni ya shirikisho ni kuwa na vyama vingi kwa kadri inavyowezekana.
Kitime ni mwanamuziki aliyeanza kazi zake rasmi mwaka 1965 na ni mmoja wa waasisi wa sheria ya haki miliki ya wanamuziki, mwaka 1993 alikuwa mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Dansi pia alishakuwa Mjumbe wa COSOTA, kwa sasa ni mwanamuziki wa bendi ya Kilimanjaro.
No comments:
Post a Comment