Wednesday, 22 June 2016

WIZARA YA ARDHI KUBAINI TAASISI ZINAZODAIWA FIDIA NA WANANCHI

Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
————————————
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika  kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017 itabaini taasisi zote na watu binafsi wanaodaiwa fidia na wananchi ili waweze kulipa fidia hizo.
Akiongea leo Bungeni, mjini Dodoma Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Angelina Mabula amesema kuwa ni kweli tatizo hilo lipo na tayari Serikali imechukua hatua kwa kuzielekeza Halmashauri zote na taasisi nyingine kulipa fidia stahiki kwa wananchi pale wanapotaka kutwaa maeneo yao.
Mhe. Mabula amesema kuwa taasisi nyingi zimekuwa zikichukua mashamba ya wananchi na kushindwa kuwalipa fidia hivyo kulimbikiza madeni hayo kwa muda mrefu hali inayokwamisha shughuli  za maendeleo.
“Halmashauri za Wilaya, Taasisi na Maafisa Ardhi hawaruhusiwi kuchukua mashamba ya wananchi kabla hawajakamilisha utaratibu wa malipo ya fidia kwa wananchi hao, ili kuondokana na malimbikizo ya madeni ya fidia ambayo malipo yake huchukua muda mrefu na kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi,” alisema Mhe. Mabula.
Aidha Mhe. Mabula amewataka wananchi wanaodai fidia kuwa wavumilivu wakati Wizara yake inaendelea kufanya upembuzi wa taasisi hizo ili ziweze kulipa fidia zote zinazodaiwa na wananchi.
Vilevile Wizara hiyo imetoa ramani za mitaa kwa wenyeviti wa mitaa wa Jiji la Dar es Salaam ili wenyeviti hao waweze kutambua matumizi ya maeneo yao, kwa mfano maeneo ya wazi, na nini kijengwe katika maeneo yao kama vile nyumba fupi au ndefu, hoteli au chuo ili kuondokana na migogoro ya kubolewa nyumba kwa kujenga eneo lisiloruhusiwa.
“Tumeanza kwa mkoa wa Dar es Salaam lakini zoezi litaendelea kila Mkoa na kila Wilaya Nchi nzima, ili Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji waweze kutambua matumizi ya maeneo yao, hivyo kuchukua hatua kwa haraka pindi ambapo maeneo hayo yanatumika tofauti na matumizi yaliyoko” alifafanua Mhe. Mabula.
Aidha Mhe. Mabula amezitaka Halmashauri kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi kuwapa uwezo wenyeviti hao ili waweze kufanya kazi hiyo kiufanisi.

No comments:

Post a Comment