Wednesday, 29 June 2016

KIWANDA CHA MBOLEA KUJENGWA WILAYANI KILWA

hog1Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akizungumza kwenye kikao na mabalozi kutoka Ujerumani na Denmark (hawapo pichani) hivi karibuni katika Ukumbi wa Wizara jijini Dar es Salaam.
hog2Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo(Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Ujerumani, Egon Kochanke(Kulia) na Balozi wa Denmark, Einar Jensen(Kushoto).
hog3Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo(Kulia) akijadiliana jambo na Balozi wa Denmark, Einar Jensen (Kushoto). Katikati ni Balozi wa Ujerumani, Egon Kochanke akiweka sahihi kwenye kitabu cha wageni ofisini kwa Waziri jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
…………………………………………………………………………………………
  • Kina thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.5
  • Kuzalisha tani milioni 1.35 kwa mwaka
Na Devota Myombe
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amekutana na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Egon Kochanke pamoja na Balozi wa Denmark nchini, Einar Jensen kujadili ujenzi wa Kiwanda cha mbolea wilayani Kilwa.
Katika mkutano huo, ilielezwa kuwa matayarisho ya ujenzi wa kiwanda hicho cha mbolea chenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.5 yanaendelea na kwamba kiwanda hicho kinatarajiwa kuzalisha tani milioni 1.35 za mbolea kwa mwaka.
Waziri Muhongo alisema ardhi kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho ipo na kuwa gesi asilia itakayotumika kiwandani hapo ipo ya kutosha.
Alisema kampuni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi zitakuwa na hisa katika kiwanda hicho ambapo kwa upande wa Tanzania, alizitaja kampuni hizo kuwa ni Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Minjingu Mines pamoja na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Aidha, kwa upande wa kampuni za nje, Profesa Muhongo alizitaja kuwa ni Ferrostaal ya Ujerumani, Haldor Topsoe ya Denmark na Fauji kutoka nchini Pakistan.
Profesa Muhongo aliwahakikishia mabalozi hao pamoja na ujumbe wao kuwa ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa kiwanda hicho ipo na kwamba gesi asilia itakayohitajika ipo ya kutosha na kuwa bado nafasi za uwekezaji zinapatikana. “Ardhi ipo, gesi ipo hivyo mnakaribishwa,” alisema Prof. Muhongo.
Naye Balozi wa Ujerumani nchini, Egon Kochanke alimshukuru Profesa Muhongo kwa kukubali kukutana na ujumbe huo kupokea maombi ya mpango wa ujenzi wa Kiwanda hicho cha mbolea ambapo alisema, hiyo ni njia mojawapo ya kuboresha uzalishaji Tanzania. “Nimefurahi sana kushiriki kikao hiki na nina kushukuru kwa kukubali kwako kupokea maombi haya,” alisema.
Kwa upande wake Balozi Einar Jensen alitumia nafasi hiyo kumshukuru Profesa Muhongo kwa jinsi alivyoupokea ujumbe huo na namna alivyoendesha majadiliano husika.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na baadhi ya watendaji wa Wizara pamoja na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini.

No comments:

Post a Comment