WAAMUZI WA MECHI SERENGETI BOYS, SHELISHELI
Waamuzi wanne kutoka Ethiopia, ndio watakaochezesha mchezo wa kimataifa kati ya timu ya Taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ na Shelisheli utakaofanyika Juni 26, 2016 kuanzia saa 10.00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo huo ni wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17. Waamuzi hao ni Belay Tadesse Asserese ambaye ni mwamuzi wa kati wakati wasaidizi wake ni Tigle Gizaw Belachew upande wa kulia na Kinfe Yilma Kinfe upande wa kushoto huku mwamuzi wa akiba atakuwa Lemma Nigussie. Kamishna wa mchezo huo atakuwa ni Bester Kalombo.
Serengeti Boys ilikuwa kambini tangu Juni 14, 2016 kujiandaa na mchezo huo wa kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya vijana wenzao wa Shelisheli utakaofanyika Juni 26, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Mchezo wa marudiano kati ya Serengeti Boys na Shelisheli utachezwa Julai 2, 2016 huko Shelisheli.
Katika kuajindaa na mchezo huo, Serengeti Boys ilifanya ziara India ambako walishiriki mashindano ya vijana ya Kimataifa yanayotambuliwa na FIFA (AIFF International Youth Tournament 2016) kabla ya kurudi na rekodi ya kupigiwa mfano si tu katika Tanzania na kwa nchi za Afrika Mashariki.
Kadhalika Serengeti Boys ilicheza mfululizo michezo saba ya kimataifa bila kufungwa dhidi ya Misri (2), India, Korea Kusini, Malaysia na Marekani (USA). Kabla ya hapo timu hiyo ilicheza michezo kadhaa ya ndani na timu za chini ya umri wa miaka 20 bila kupoteza hata mchezo mmoja.
Katika mashindano ya AIFF, timu hiyo pekee kutoka Afrika na ambayo ilikua kipenzi cha mashabiki katika jiji la Goha ilicheza na timu ambazo ziko juu katika hatua za juu katika mtoano wa kuwania kushiriki Kombe la Dunia kupitia mabara yao yaani CONCACAF (USA) na AFC (India, Korea na Malaysia).
Awali timu ya Serengeti Boys ilipewa nafasi ndogo ya kufanya vizuri kwa sababu ya rekodi zilizokuwa zinaiweka Tanzania katika viwango vya chini katika umri huo kwa nchi za Afrika Magharibi na Kaskazini zilikuwa juu zaidi na vilevile ukweli wa kwamba timu kama USA, Korea, Malasyia na India zilikuwa na bajeti kubwa iliyogharamiwa na Serikali zao na walikuwa na vifaa vya kila namna kiasi cha kuomba magari kwa ajili ya vifaa vya mazoezi na mechi.
Serengeti Boys ilimaliza Mashindano ya AIFF katika nafasi ya tatu kwa kuifunga Malaysia mabao 3-0. Serengeti Boys na Bingwa Korea hawakupoteza mchezo hata mmoja na awali walipokutana walitoka sare ya 2-2
MWAMUZI WA ANGOLA KUWAAMUA YOUNG AFRICANS, TP MAZEMBE
Mchezo wa kuwania Kombe la Shirikisho Barani Afrika kati ya Young Africans ya Dar es Salaam, Tanzania na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), utachezeshwa na Mwamuzi Janny Sikazwe wa Zambia
Sikazwe atasaidiwa na Jarson Emiliano dos Santos kutoka Angola atayekuwa kwenye mstari wa kulia (line 1) na Berhe O’Michael wa Eritrea atayekuwa upande wa kushoto (line 2) huku Wellington Kaoma wa Zambia akiwa ni mwamuzi wa akiba. Kamishna wa mchezo huo atakuwa Celestin Ntangungira wa Rwanda. Pia mchezo huo utakuwa na Mratibu Mkuu Maalumu kutoka Msumbiji, Sidio Jose Mugadza.
SUALA LA STAND UNITED YA SHINYANGA
Kutokana na mkanganyiko wa uendeshaji wa mchakato wa uchaguzi katika Klabu ya Stand United ya Shinyanga, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF), limeagiza michakato yote miwili inayoendeshwa sambamba ndani ya klabu ya Stand United, isimamishwe mara moja kisha kusubiri maelekezo mengine.
No comments:
Post a Comment