Thursday, 16 June 2016

OSHA KUJA NA MBINU MPYA ZA KUWASAIDIA WAFANYAKAZI




Washiriki wa mafunzo hayo wakimsikiliza mwendeshaji wa mafunzo hayo, Andrew Christian ambaye yupo Geneva, Switzerland aliyekuwa akitoa elimu kuhusu ukaguzi kwa wafanyakazi
 
Wakiwa kama wakaguzi wa huduma za afya na usalama kwa wafanyakazi katika maeneo ya kazi, Wakala wa Afya na Usalama sehemu za Kazi (OSHA) wameeleza kuwa wataboresha ukaguzi wao hasa kwa wafanyakazi walio na UKIMWI jinsi wanavyohudumiwa na waajiri wawapo kazini.

Akizungumza na Mo Blog katika mafunzo ya jinsi ya kufanya kaguzi sehemu za kazi kwa watu walio na UKIMWI, Kaimu meneja usajili na takwimu za afya na Usalama OSHA, Dk. Abdalssalaam Omary, alisema kupitia mafunzo hayo wanataraji kuboresha ukaguzi zao ambazo zifanywa katika maeneo ya kazi ambazo zinakuwa zinawahusu watu walio na UKIMWI.

“Tunaamini kuwa baada ya mafunzo tutakuwa na maboresho katika kaguzi zetu sababu tumepata nafasi ya kukutana na wenzetu kutoka sehemu nyingine na kubadilishana uelewa kwahiyo tutakuwa tofauti na awali,” alisema Dk. Omary.

Alisema pamoja na kujipanga kuboresha kaguzi zao alisema kuwa bado wamekuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo kwa muda mwingine zinaweza kuwa zinawafanya wakwame na kueleza changamoto hizo ni pamoja na fedha na madaktari kwa ajili ya kuwafanyia uchunguzi wafanyakazi.

Kwa upande wa serikali kupitia Kaimu Kamishna wa Kazi Msaidizi, Rehema Moyo alisema kuna sheria ambazo zimewekwa ambazo zinakataza waajiri kufanya vitendo vya ubaguzi kwa wafanyakazi na hivyo kama kuna waajiri wanawafanyia vitendo ambavyo havikubaliki kisheria basi watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakani kujibu mashitaka yanayowakabili.

“Sera zipo utekelezaji ndiyo mgumu kuna vitendo vya ubaguzi lakini kujua ndiyo inakuwa changamoto maana ni mpaka muhusika aseme na sheria zipo kama mwajiriwa akikutwa na hatia anaweza hata kufungwa gerezani au kupigwa faini,” alisema Bi. Moyo.

Nae Mratibu wa maswala yanayohusiana na UKIMWI maeneo ya kazi kutoka Shirika la Kazi (ILO), Getrude Sima, alisema kupitia mafunzo hayo wanaamini washiriki wataweza kupata kitu kipya ambacho kitawasaidia katika kaguzi wanazozifanya ili waweze kutambua zaidi matatizo yanayowakuta wagonjwa wa UKIMWI wawapo kazini na jinsi ya kuwasaidia.
.

No comments:

Post a Comment