Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umekabidhi kituo cha Uchunguzi na Matibabukwa Hospitali ya Rufaa Dodoma kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kupata huduma bora za matibabu.
Kituo hicho kimekabidhiwa leo mkoani Dodoma na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Benard Konga kikiwa na lengo la kuwapa wananchi huduma bora za matibabu na kuweka wataalamu wenye uzoefu ili iwe ni sehemu ya kujifunzia kwa wataalamu wa kada mbalimbali za udaktari.
“Kituo hiki kimejengwa kisasa kwa kuwekewa mfumo wa kisasa wa miito ya manesi (Nurse Call System), jengo la jenereta na transfoma kwa ajili ya kuwa na umeme wa uhakika masaa yote, mifumo ya kisasa ya vipooza hewa, sehemu ya mapokezi, sehemu ya kutolea dawa, sehemu ya dharura, maabara, vyumba vya uchunguzi, vyumba vya Madaktari, chumba cha upasuaji, chumba cha wagonjwa mahututi, kliniki mbalimbali,sehemu za kulaza wagonjwa zenye jumla ya vitanda 34 pamoja na Jengo la mgahawa kwa ajili ya huduma ya chakula”alisema Konga.
Konga ameongeza kuwa kuna baadhi ya shughuli za ujenzi zinaendelea kukamilishwa lakini haziwezi kuzuia kuanza kufanya kazi kwa kituo hicho kwa sababu huduma hizo zinapatikana katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ambayo inasimamia kituo hiko.
Aidha, Konga amezitaja baadhi ya shughuli za ujenzi zinazoendelea zikiwemo jengo la kuhifadhia maiti,ujenzi wa sehemu ya kufulia nguo pamoja na sehemu ya kuchomea taka ambazo amekiri kuwa hazitachukua mda mrefu kukamilika kwakua fedha za ujenzi huo zilishatengwa.
Amefafanua kuwa Mfuko huu una mpango wa kuimarisha huduma kwa kujenga vituo kama hivi katika kila Kanda na kwa mwaka wa fedha 2016/2017 mfuko umepanga kujenga kituo kama hiki mkoani Kigoma.
Mradi wa ujenzi wa Kituo hicho ulianza mwezi Oktoba, 2009 ambapo ujenzi wa jengo umegharimu zaidi ya shilingi Bilioni 6.Jumla ya shilingi Bilioni 2 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya vifaa tiba na samani.
No comments:
Post a Comment