Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza
jambo na mwenyeji wake Rais Mteule wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni
mara baada ya kuwasili katika Ikulu ya Uganda.
……………………………………………………………………………………………………………………….
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 11 Mei, 2016 amewasili
Jijini Kampala nchini Uganda ambapo kesho anatarajiwa kuhudhuria sherehe
za kuapishwa kwa Rais Mteule wa Jamhuri ya Uganda Mheshimiwa Yoweri
Kaguta Museveni.
Rais Magufuli ametua katika
uwanja wa ndege wa Entebe majira ya saa tano za asubuhi na kupokelewa na
Waziri wa Ujenzi na usafirishaji wa Uganda Mheshimiwa John Byabagambi
na kisha kuelekea Ikulu ya Entebe ambako amepokelewa rasmi na mwenyeji
wake Mheshimiwa Rais Yoweri Kaguta Museveni.
Akiwa katika Ikulu ya Entebe Rais Magufuli amekagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa heshima yake na pia amepigiwa mizinga 21.
Aidha, Viongozi hao wamefanya
mazungumzo ambapo pamoja na kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano
na uhusiano kati ya nchi hizo mbili, Rais Magufuli amemhakikishia Rais
Museveni kuwa Tanzania itatoa ushirikiano wa kutosha kufanikisha ujenzi
wa bomba la mafuta linalotarajiwa kujengwa kutoka Hoima katika Ziwa
Albert nchini Uganda na kupita kaskazini mwa Tanzania hadi bandari ya
Tanga.
Rais Magufuli ameongozana na
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda
na Kimataifa Mheshimiwa Suzan Kolimba.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Kampala
11 Mei, 2016
No comments:
Post a Comment